• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Msimamizi wa Bajeti kushtakiwa kwa makosa anayodaiwa kufanya 2016

Msimamizi wa Bajeti kushtakiwa kwa makosa anayodaiwa kufanya 2016

NA ANTHONY KITIMO

Msimamizi wa Bajeti Margaret Nyakang’o na watu wengine 10 wanatazamiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuhusiana na kesi iliyofunguliwa kuhusiana nao mnamo 2016.

Washukiwa hao 11 wanatarajiwa kushtakiwa kwa makosa mbali mbali, likiwemo lile la kupanga kulaghai mahakama ya Mombasa.

Aidha, watashtakiwa pia kwa kuendesha shirika la akiba na mikopo (Sacco) bila leseni, na kuwasilisha stakabadhi ghushi.

Mashtaka hayo yameidhinishwa na afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma, ODPP, kwenye barua iliyotumwa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi (DCI) Novemba 30.

Kulingana na stakabadhi ambazo Taifa Leo imeziona, Naibu DPP Jacinta Nyamosi anasema kundi hilo la watu 11 lina kesi ya kujibu.

“Tumepokea barua yako yenye usajili DCI/SEC/LCA/4/4/16/Vol. VII/24 ya Oktoba 31, 2023 inayowasilisha tena upelelezi kuhusu jambo hili na inahitaji mwelekeo,” Bi Nyamosi anasema.

Akaongeza: “Tunatambua kwamba faili hiyo iliwasilishwa kwa mara ya kwanza Julai 6, 2022 na baada ya kuikagua, ilipatikana ina sehemu ambazo zilihitaji kushughulikiwa…”

Wengine ambao wanatarajiwa kufunguliwa mashtaka ni Jackson Ngure Wanjau, Susan Kendi, James Makena Wanyagi, John Muchira Kithaka, Jane Karuu Ndanyi na Muthoni Elphas, Joan Chumo, Mercy Ndura Mukosa, Gregory Mwangangi Mailu na Michael Kipkurui.

“Faili imeletwa tena kwa ODPP na baada ya upekuzi na ushahidi mpya, tumeona kwamba washukiwa wanastahili kufunguliwa mashtaka ya pamoja,” akasema Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

  • Tags

You can share this post!

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama atishiwa...

Waliohusika na sheria dhidi ya ushoga Uganda kunyimwa...

T L