• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Mswada wa Fedha wa 2023 kuchangia kupanda kwa bei ya unga – KAM

Mswada wa Fedha wa 2023 kuchangia kupanda kwa bei ya unga – KAM

NA CHARLES WASONGA

BEI ya unga inatarajiwa kuendelea kupanda ikiwa wabunge watapitisha Mswada wa Fedha wa 2023.

Hii ni kufuatia pendekezo kwenye mswada huo la serikali kuanzisha ushuru wa kima cha asilimia 10 kwa karatasi inayotumika kupakia unga na bidhaa nyinginezo za chakula.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari mnamo Alhamisi, Mei 25, 2023, Chama cha Watengenezaji Bidhaa Nchini (KAM) kilisema kuwa kuanzishwa kwa ushuru huo kutaathiri bei ya unga.

“Hii itachangia bei ya unga kuongezeka zaidi wakati kama huu ambapo wananchi wanakabiliwa na wakati mgumu kufuatia kupanda kwa gharama ya maisha,” KAM ikasema.

Serikali inaanzisha ushuru huo kwa karatasi ya kutengeneza mifuko ya kupakia unga na vyakula vinginevyo wakati ambapo Wakenya wanalalamikia bei ya juu ya unga, sukari na bidhaa nyinginezo za kimsingi.

Tangu Januari 2023 viongozi wa upinzani wamekuwa wakiishinikiza serikali ya Kenya Kwanza ipunguze bei ya unga hadi Sh100 kwa paketi moja ya kilo mbili ilivyoahidi wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Mnamo Machi 2023 vinara wa Azimio la Umoja-One Kenya waliitisha maandamano katika miji mbalimbali nchini wakilalamikia mambo mbalimbali ikiwemo bei ya juu ya unga.

Mnamo Aprili 12, 2023 Rais William Ruto alitangaza kuwa bei ya unga ingeshuka hadi Sh150 kwa paketi moja ya kilo mbili. Hii ni baada ya sehemu ya magunia milioni 10 ya mahindi ambayo serikali ya Kenya Kwanza iliagiza kutoka ng’ambo kuanza kuwasili nchini kupitia bandari ya Mombasa.

Lakini licha ya tangazo hilo, bei ya unga imesalia juu ambapo bidhaa hiyo inauzwa kwa kati ya Sh190 na Sh240 kwa paketi ya kilo mbili katika maduka mengi ya jumla jijini Nairobi na viunga vyake.

Aidha, mswada huo wa Fedha wa 2023 unapendekeza ushuru wa adhabu (excise duty) ya Sh5 kwa kilo ya sukari.

Utozaji wa ushuru huo pia utachangia ongezeko la bei ya sukari kuliko ilivyo sasa ambapo bei ya sukari ni Sh220 kwa kilo moja.

Bei ya sukari imekuwa ikipanda nchini kutokana na kupunguka kwa uzalishaji. Hii, wadau, katika sekta hiyo wanasema ni kutokana na hali ya kiangazi cha muda mrefu iliyoshuhudiwa nchini.

  • Tags

You can share this post!

Isuzu yazindua gari la kipekee ‘Eliud Kipchoge 1:59...

Sumu kali ndani ya Mswada wa Fedha

T L