• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Mtihani kwa Uhuru kipindi cha lala salama

Mtihani kwa Uhuru kipindi cha lala salama

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta leo Jumanne anatarajiwa kuangazia mikakati ya serikali ya kukabiliana na changamoto zinazolikumba taifa sasa kama vile ukame, janga la Covid-19 na kupanda kwa gharama ya maisha, miongoni mwa nyingine kwenye hotuba yake ya hali ya taifa.

Kwenye hotuba atakayotolea bungeni alasiri, Rais Kenyatta pia anatarajiwa kuzungumzia maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 9, 2022.

Huku kampeni za urithi wa kiti chake zikiwa zimeshika kasi, na mawaziri wake wakilaumiwa kwa kuegemea mrengo fulani katika mchakato huo, kiongozi taifa anatarajiwa kutoa kauli yake kuhusu suala hilo. Rais Kenyatta anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho ambapo kikatiba, anatarajiwa kustaafu baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga ni miongozi mwa wanasiasa ambao wamejitokeza kutaka kurithi kiti hicho.

Lakini chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho Dkt Ruto ametangaza atakitumia kuwania kiti hicho, kimelalamikia kushirikishwa kwa Mawaziri Fred Matiang’i na Joe Mucheru katika kamati maalum ya kuongoza maandalizi ya uchaguzi huo kikidai wanampendelea Bw Odinga.

“Rais anatarajiwa kuangazia jambo hilo kwa sababu linahusisha mawaziri wake mbali na kuibua hofu kwamba uchaguzi mkuu hautaendeshwa kwa njia huru na haki,” akasema Seneta wa Meru Mithika Linturi, ambaye ni mmoja wa wandani wakuu wa Dkt Ruto.

Lakini mwanauchumi Tony Watima alielezea matumaini kuwa Rais Kenyatta atatenga muda mwingi kuorodhesha mafanikio yaliyopatikana na utawala wake na changamoto zilizoukumba.

“Kwa mfano, Rais Kenyatta anatarajiwa kudurusu utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu za Maendeleo. Atataja changamoto zilizozuia utekelezaji wa baadhi ya nguzo za ajenda hii na mipango ya kukabiliana na changamoto hizo ndani ya miezi tisa iliyosalia kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” anasema.

“Baadhi ya changamoto hizo bila shaka ni ufisadi, ukame na janga la Covid-19 lililochipuka nchini Machi 13, 2020. Wakenya watasubiri kwa hamu kusikia mikakati zaidi ambayo Rais Kenyatta atatangaza kwa ajili ya kukarabati uchumi ulioathiriwa na changamoto hizi,” Bw Watima anaongeza.

Katika hotuba yake wakati wa sherehe za Mashujaa Dei Oktoba 20, 2021 katika uwanja wa Wang’uru, Kaunti ya Kirinyaga, Rais Kenyatta alitangaza mpango wa ukarabati wa sekta mbalimbali za uchumi kwa gharama ya Sh10 bilioni.

Vile vile, Rais Kenyatta aliondoa kafyu ili kutoa nafasi kwa Wakenya kuendelea na shughuli zao za kawaida zilizodhibitiwa ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Hii ni baada ya Kenya kuanza kuandikisha visa vichache vya maambukizi ya ugonjwa huo hatari kufuatia kampeni ya utoaji chanjo iliyoendeshwa na serikali. Hata hivyo, Rais Kenyatta aliwahimiza Wakenya kuendelea kuzingatia masharti ya kuzuia msambao wa corona na wajitokeze kwa wingi kupokea chanjo za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.

Leo kiongozi wa taifa anatarajiwa kuendeleza himizo hilo kufuatia kuchipuza kwa aina mpya ya Covid-19 kwa jina Omicron. Aina hiyo ya kirusi iligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini, mwezi huu Novemba.

Wataalamu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) wanasema kuwa kirusi hicho ambacho kimeenea katika mataifa kadha kusini mwa Afrika ni hatari kuliko Delta kilichogunduliwa nchini India mapema mwaka 2021.

You can share this post!

Askofu Ole Sapit asimama imara kuzima siasa kanisani

Dhuluma za ngono zinavyotatiza utalii

T L