• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Muchai aliuawa na jambazi sugu chini ya dakika moja, mahakama yaambiwa

Muchai aliuawa na jambazi sugu chini ya dakika moja, mahakama yaambiwa

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Mbunge wa Kabete George Muchai, walinzi wake wawili, na dereva wake waliuawa na majambazi waliotumia bunduki ya serikali aina ya G3 ambayo walimnyang’anya polisi mwaka 2014 katika eneo la Kitisuru, Nairobi.

Mahakama imeambiwa Muchai aliuawa chini ya nusu dakika na jambazi aliyekuwa amekubuhu kwa uhalifu.

Muchai, walinzi wake Konstebo Samwel Lekakeny na Konstebo Samwel Kimathi na dereva wake Stephen Wambugu, walimiminiwa risasi tano na jambazi Eric Isabwa almaarufu Chairman kando ya barabara ya Kenyatta Avenue katika eneo mkabala na GPO Februari 7, 2015.

Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Kanyi Kimondo, afisa wa upelelezi wa jina Sajini Moses Otiu Opiyo, alifichua kwamba bunduki  iliyotumika kuwaangamiza Muchai, Lekakeny, Kimathi na Wambugu ilikuwa imenyang’anywa kutoka kwa Koplo Patrick Wamae mnamo Oktoba 2014 katika eneo la Kitisuru akilinda jengo la serikali.

Sajini Opiyo alieleza Jaji huyo bunduki hiyo ya G3 na bastola aliyong’anywa Konstebo Lekakeny ndizo silaha zilizopatikana katika makazi ya Isabwa na mkewe Margaret Njeri.

Polisi walipata bunduki hiyo katika makazi ya Isabwa na Njeri yaliyoko Kinoo.

Sajini Opiyo alieleza mahakama kwamba Isamba na jambazi mwingine Raphael Kimani walikuwa wamevalia maski kwenye nyuso zao walipomwangamiza Muchai ambaye wakati huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini-COTU.

Baada ya kuwaua wanne hao, Isabwa na Kimani walimpigia dereva wa teksi simu kuwaondoa haraka.

“Baada ya mauaji ya Muchai na wenzake, Kimani alimpigia simu dereva wa teksi kuja kuwachukua kutoka GPO,” alisema Sajini Opiyo.

Afisa huyo wa upelelezi alimweleza Jaji Kanyi Kimondo kwamba Isabwa na Kimani wako na rekodi ya kufungwa miaka minane gerezani kwa wizi wa mabavu.

“Nilichunguza kutoka kwa idara ya kupeleleza uhalifu na kupata historia ya Isabwa na Kimani kwamba waliwahi kufungwa jela kwa wizi wa mabavu,” Sajini Opiyo alimweleza Jaji Kimondo.

Mbali na Isabwa, Kimani na Njeri, washtakiwa wengine ni Simon Wambugu Gachamba, Stephen Lipapa, Mustafa Maina Wanyonyi na Jane Wanjiru almaarufu Shiro.

Walipokamatwa, polisi walimpata Isabwa na simu 10 za kiunga mbali, Wanjiru naye alikuwa na simu 14  za kiunga mbali na Kimani alikuwa na simu 10.

Washtakiwa hao saba wamekana waliwaua Muchai, Lekakeny, Kimathi, na Wambugu.

Washukiwa hao wa ujambazi walikuwa wamewateka nyara watu watatu na kuwasukuma ndani ya buti ya gari yao muundo wa Mercedes Benz.

Walitumia Benz hiyo kuwaandama Muchai na wenzake kutoka Westlands alipokuwa ameenda kumnunulia mkewe na watu wengine wa familia yake maankuli ya jioni.

  • Tags

You can share this post!

Ni kufa kupona Harambee Starlets wakishuka dimbani dhidi ya...

Ndege yapata panchari ikitaka kupaa Manda

T L