• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Mudavadi awasihi mahasla wavumilie ushuru wa juu

Mudavadi awasihi mahasla wavumilie ushuru wa juu

NA PHILIP MUYANGA

KINARA wa Mawaziri Musalia Mudavadi (pichani) mnamo Jumatano aliwataka Wakenya wawe wavumilivu na kuridhia kuongezewa ushuru, akisema kuwa hiyo ndiyo njia pekee ambayo serikali itapata pesa za kugharimia huduma kwa raia.

Bw Mudavadi aliunga mkono Mswada wa Fedha wa 2023 ambao unalenga kuongeza ushuru ikiwemo ushuru wa asilimia 16 kwenye mafuta.

Bw Mudavadi alisema Wakenya wanastahili kujifunga mikanda zaidi kwa sababu hali ya uchumi kwa sasa hauruhusu serikali kutoa huduma.

Kiongozi huyo ambaye amewahi kuhudumu kama waziri wa fedha wakati wa utawala wa Kanu, alikiri kuwa Wakenya wanaumia ila akasisitiza kuwa serikali haina jingine ili kusaka pesa za kuendesha shughuli zake.

“Hakuna suluhu rahisi. Tutaumia kwa muda wa miaka miwili lakini baadaye, gharama ya maisha itashuka chini. Mikakati ambayo imekumbatiwa na serikali kufufua uchumi ni magumu ila ukweli ni kwamba itanusuru raia baada ya kipindi fulani,” akasema Bw Mudavadi.

Waziri huyo alisema kuwa deni la ushuru ambalo halijalipwa hadi sasa ni Sh1.5 trilioni. Pia thamani ya sarafu ya Kenya imeshuka huku deni la nchi likiwa Sh10 trilioni.

Alikuwa akizungumza baada ya kufungua Kongamano la Taasisi za Mahasibu Nchini (ICPAK) jijini Mombasa ambako alisema kuwa serikali haiwezi kuendelea kukopa na kuwaongezea Wakenya mzigo wa deni.

Kwa kusema kuwa uchumi utaimarika baada ya miaka miwili, Bw Mudavadi ana imani hilo litafanyika kutokana na utathmini wake wa hali ya sasa ambapo alisema uchumi unaelekea kusambaratika.

  • Tags

You can share this post!

Hospitali ya watoto ya Gertrude’s yaahidi kuboresha...

Azimio yataka msajili wa vyama vya kisiasa atoke

T L