• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 12:05 PM
Musalia afunika Gachagua

Musalia afunika Gachagua

NA WANDERI KAMAU

MKUU wa Mawaziri Musalia Mudavadi anaonekana kuwa Balozi Mkuu wa Rais William Ruto kimataifa, akifanya ziara muhimu kimataifa kumwakilisha Rais.

Ijapokuwa kiitifaki Naibu Rais Rigathi Gachagua ndiye wa pili kimamlaka kutoka kwa Rais na ndiye anayefaa kumwakilisha katika hafla kama hizo, Rais Ruto ameonekana kumtwika jukumu hilo Bw Mudavadi, hali ambayo imeibua maswali.

Tangu Desemba 2022, Bw Mudavadi amekuwa akifanya ziara muhimu nje ya nchi kumwakilisha Rais Ruto katika mikutano na makongamano ya ngazi za juu.

Jumatatu wiki iliyopita, Bw Mudavadi alimwakilisha Rais Ruto nchini Nigeria, wakati wa hafla ya kuapishwa kwa rais mpya wa Nigeria, Bola Tinubu.

Kwenye ziara hiyo, Bw Mudavadi alimpa pongezi Bw Tinubu kwa ushindi wake kwa niaba ya serikali ya Kenya, huku akimwahidi kuwa “Kenya imejitolea kuimarisha uhusiano baina yake na Nigeria kwa manufaa ya mataifa hayo mawili”.

Mnamo Ijumaa, Bw Mudavadi, alisafiri tena jijini Luanda, Angola, kumwakilisha Rais Ruto kwenye Kongamano la Mataifa Wanachama wa Mwafaka wa Kurejesha Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na eneo la Maziwa Makuu.

Bw Mudavadi pia huongoza ujumbe wa Kenya. Desemba mwaka uliopita, alimwakilisha Rais Ruto katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Mataifa Wanachama wa Jumuiya ya Madola, jijini London, Uingereza.

Mwaka huo huo aliandamana na Rais Ruto kwenye ziara nchini Amerika kuhudhuria Kongamano Baina ya Viongozi wa Afrika na Amerika.

Machi 2022, Bw Mudavadi alimwalikisha Rais Ruto katika kongamano la Nchi Zisizoegemea Upande Wowote (NAM), nchini Azerbaijan.

Kabla ya hapo, alikuwa amemwakilisha Rais katika hafla ya kuapishwa kwa Rais Lula Inacio da Silva wa Brazil.

Mwezi Aprili 2022, Bw Mudavadi alimwakilisha Rais Ruto katika kongamano maalum kuhusu mikakati ya kutafuta amani nchini DRC Congo jijini Bunjumbura, Burudi.

Hali hii inafanya wadadisi kusema kuwa ingawa Rais Ruto amemdumisha Bw Gachagua kama Naibu Rais, anaonekana kumtegemea pakubwa Bw Mudavadi kuendeleza ajenda ya Kenya kimataifa.

Wanaamini japokuwa Bw Mudavadi ana tajriba pana serikalini, huenda kuna mpango fiche kuhusu siku za usoni.

“Tunajua ana tajriba pana katika masuala ya uongozi na uendeshaji serikali ikilinganishwa na viongozi wengine walio katika serikali ya Rais Ruto, lakini huenda kuna mpango wa kumjenga kisiasa. Pili, huenda rais anampendelea kutokana na siasa na sifa zake za kiungwana,” asema mdadisi wa siasa Bw Kipkorir Mutai.

Hata hivyo, mdadisi Macharia Munene anasema ni mapema kusema kuna mpango wa kumjenga kisiasa Bw Mudavadi.

“Ni mapema mno kudai kuwa Rais anamjenga kisiasa Bw Mudavadi. Ikumbukwe kuwa, Rais Ruto bado anaendelea kuweka msingi wa kiutawala, kisiasa, kiuchumi na kimataifa wa serikali yake. Ushirikiano mzuri baina yake na jamii ya kimataifa ni nguzo muhimu sana ambayo itamsaidia kutimiza baadhi ya malengo na mipango yake. Katika kutimiza hilo, lazima amtumie mtu mwenye tajriba pana katika masuala ya utawala. Nadhani ndipo Bw Mudavadi anapoingia,” akasema jana, Jumamosi, Juni 3, 2023 kwenye mahojiano na ‘Taifa Jumapili.’

Wakati wa kampeni za mrengo wa Kenya Kwanza 2022, Rais Ruto aliahidi “kumrejeshea mkono” Bw Mudavadi kwa hatua yake kumuunga mkono.

Baadhi ya wadadisi wanataja uamuzi wa Rais kama njia ya kutimiza ahadi hiyo.

Wengine wanasema kuwa litakuwa kosa kwa Rais Ruto kuanza kumjenga kisiasa Bw Mudavadi, wakidai ni mapema sana.

Katika Agizo la Kulainisha Utendakazi wa Serikali alilotoa Januari 2022, Rais Ruto alionekana kumkweza Bw Mudavadi, kwa kumpa majukumu muhimu kama usimamizi na ushirikishi wa utendakazi katika wizara zote za serikali.

  • Tags

You can share this post!

Pigo kuu Pasta Ezekiel akizuiwa kuhudhuria mkutano wa injili

Akothee na mumewe, fungate yapamba moto

T L