• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 4:21 PM
Mwalimu akatwa na mbawa za helikopta Garissa na kufariki

Mwalimu akatwa na mbawa za helikopta Garissa na kufariki

NA MANASE OTSIALO

Naibu Mwalimu Mkuu ameuawa baada ya kukatwa kichwani na mbawa za helikopta.

Kisa hicho cha Novemba 21, 2023 asubuhi kilifanyika eneo la Masalani, katika kaunti ndogo ya Ijara, Kaunti ya Garissa.

Akithibitisha kisa hicho, Kamishna wa Kaunti ya Garissa Solomon Chesut alisema bado haijabainika kuhusu kilichomfanya mwendazake akaribie helikopta hiyo iliyokuwa inajiandaa kupaa.

“Kumekuwa na kisa ambapo mwalimu alifariki papo hapo baada ya kukatwa na mbawa za helikopta. Tumeanzisha uchunguzi kubaini alichokuwa akifanya karibu na helikopta,” akasema Bw Chesut.

Mkuu huyo wa kiusalama Garissa alitaja tukio hilo kuwa la kusikitisha.

“Marehemu aamekuwa akifungua makasha ya mtihani katika afisi ya DCC,” akasema.

Walioshuhudia wanasema walimu huyo alikimbilia kuabiri ndege hiyo kwa kuwa alikuwa anahusika katika usambazaji wa mitihani katika shule mbali mbali katika kaunti ndogo ya Ijara.

Sehemu nyingi za Garissa zimekuwa zikifurahia huduma za helikopta katika usambazaji wa mitihani baada ya barabara kukosa kupitika kutokana na mafuriko ya mvua ya El Nino.

Helikopta mbili ambazo zinahudumu Garissa pia hutumika katika kaunti jirani ya Tana River.

Kaunti tatu za Kaskazini Mashariki zina helikopta mbili kila moja zinazotumika katika usambazaji wa mtihani wa KCSE unaoendelea.

Wajir imebakia na helikopta moja baada ya nyingine kuanguka Jumatatu Novemba 20, asubuhi ilipokuwa inaondoka uwanja wa ndege wa Wajir.

Soma kisa hicho hapa: https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/ndege-mbili-za-helikopta-zahusika-katika-ajali-tofauti-wajir

Takriban watu watatu akiwemo rubani na mwanasiasa wa eneo hilo walijeruhiwa katika mkasa huo na kukimbizwa hospitalini.

Helikopta nyingine ya jeshi ilianguka vile vile katika eneo la Buna, Wajir Kaskazini hiyo hiyo Jumatatu ilipokuwa inasambaza msaada kwa wahanga wa mafuriko.

Katika taarifa, Jeshi lilisema kwamba wote waliokuwemo kwenye ndege hiyo waliponyoka bila majeraha na kwamba uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha ajali hiyo huku wakazi wakisema wanashuku ilikuwa imebeba mizigo kupita kiasi.

 

  • Tags

You can share this post!

Pwani yazama El Nino ikitishia kunyima hoteli mahanjam ya...

Ruto alituenjoi kuhusu mapato ya Tsavo, asema Seneta wa...

T L