• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama atishiwa maisha na majangili anaolenga kuzima Rift Valley

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama atishiwa maisha na majangili anaolenga kuzima Rift Valley

NA CHARLES WASONGA

MWENYEKITI  wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama Gabriel Tongoyo ameshikilia kuwa kamati hiyo itaendelea kuchunguza chanzo cha utovu wa usalama Kaskazini mwa Kenya licha ya vitisho anavyopokea kutoka kwa baadhi ya “wadhamini” wa visa hivyo.

Akiongea wakati kamati yake ilikutana na wabunge kutoka kaunti za Samburu na Turkana Bw Tongoyo alifichua kuwa amekuwa akipokea simu zenye jumbe za kumtishia maisha kutoka kwa watu fulani wakimwonya dhidi ya kuendeleza uchunguzi kuhusu visa vya ujangili na wizi wa mifugo katika eneo la North Rift.

“Sikutaka kufichua hili wakati huu, lakini ninataka kuwaambia kuwa nimekuwa nikipokea vitisho vya kifo kutoka kwa watu wanaonipigia simu wakinionya kuhusu uchunguzi unaoendelea kuhusu kiini cha utovu wa usalama haswa wizi wa mifugo kaskazini mwa Kenya,” Mbunge huyo wa Narok Magharibi akasema wakati wa kikao na wabunge hao katika majengo ya Bunge jijinu Nairobi mnamo Ijumaa.

Wabunge waliofika mbele ya kamati hiyo ni; Naisula Lesuuda (Samburu Magharibi, John Ariko (Turkana Kusini), Protus Akuja (Loima), Paul Nabuin (Turkana Kaskazini) na Joseph Namuar (Turkana ya Kati).

Bw Tongoyo, hata hivyo aliwahakikishia wabunge hao kuwa hatagutushwa na vitisho hivyo na kuapa kwamba kamati yake itaendelea na uchunguzi kuhusu visa hivyo.

“Kufikia sasa tumeendesha uchunguzi wetu katika kaunti za Samburu na Turkana na sasa tutaendelea katika kaunti ya Pokot Magharibi. Lengo letu ni kubaini chanzo cha visa hivyo, kisha kuandaa ripoti itakayowasilishwa kwa serikali kwa utekelezaji,” akaeleza.

Wakati wa kikao hicho, wabunge wa kaunti ya Turkana waliitaka serikali kuwapeleka wanajeshi wa KDF katika maeneo ya mpaka wa Kenya na Uganda ili kupambana na visa vya uhalifu.

Hata hivyo, Bi Lesuuda alielezea Kamati hiyo jinsi ambavyo majangili na wezi wa mifugo huhangaisha wakazi wa Samburu Magharibi licha ya kuwepo kwa kambi ya KDF katika eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

El-Nino: Gachagua, magavana waendelea kupakana tope

Msimamizi wa Bajeti kushtakiwa kwa makosa anayodaiwa...

T L