• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 12:43 PM
Mzee wa jamii ya Boni adai hakuna cha kujivunia Madaraka Dei

Mzee wa jamii ya Boni adai hakuna cha kujivunia Madaraka Dei

NA KALUME KAZUNGU

HUKU Kenya ikiadhimisha miaka 60 tangu kupata uhuru (Madaraka) kutoka kwa Mkoloni, mzee Badaa Abala,80, kwake hakuna cha kujivunia.

Yeye ni mmoja wa Wakenya wanaotoka kwa jamii ya walio wachache ya Boni ambao makao au ngome yao kuu ni msitu wa Boni katika Kaunti ya Lamu.

Akizungumza na Taifa Leo kijijini kwao Mararani, msituni Boni Jumatano, Mzee Abala, ambaye pia ni baba wa watoto wanne anasema hana la kujivunia wala kusherehekea miaka yote iliyopita ya uhuru.

Kenya ilipata uhuru mwaka 1963 wakati Rais wa kwanza nchini Kenya, hayati Mzee Jomo Kenyatta, alipoapishwa kuwa Waziri Mkuu.

Kwa kawaida, Madaraka Dei husherehekewa katika sehemu mbalimbali nchini Kenya.

Wakenya hupata fursa kuonyesha ukomavu wa uhuru, iwe ni kupitia nyimbo za kizalendo, za burudani na maonyesho na maigizo mbalimbali.

Ila kwa mzee Abala, Madaraka Dei anaihisi sawa na siku nyingine zozote, akitaja njaa inayokabili jamii ya Waboni, umaskini, ukosefu wa hatimiliki za ardhi, kukosa vitambulisho, miundomsingi duni, elimu duni, ugumu wa kupata huduma bora za afya na utovu wa usalama kuwa baadhi ya mambo yanayoendelea kuwazonga na kuwakosesha uhuru.

Mzee Abala anashikilia kuwa uhuru kwake unamaanisha afya na lishe bora kwa wananchi, miundomsingi mwafaka, wananchi kumiliki hatimiliki, watoto kupata elimu bora, usalama kuboreshwa na barabara kuimarishwa miongoni mwa haki nyingine za kimsingi kutimizwa.

“Yasikitisha kwamba tuko karne ya 21 lakini hakuna Mboni hata mmoja, hasa sisi tunaoishi vijiji vilivyoko ndani ya msitu wa  Boni amekabidhiwa hatimiliki ya ardhi. Twaadhimisha miaka 60 ya uhuru kweli lakini mimi na jamii yangu hatuna la kujivunia,” akasema Bw Abala.

Mzee huyo ambaye pia ni mmoja wa maafisa wa Nyumba Kumi kijijini Mararani pia alilalamikia ubaguzi wa wazee kutoka jamii yake katika ugavi wa fedha za wazee kutoka kwa serikali ya kitaifa.

“Tulisikia tu kwamba wazee wa umri wa miaka 70 kuendelea watakuwa wanapewa Sh2,000 kila mwezi lakini kwetu hiyo ni ndoto. Hata kusajiliwa bado. Tunasikia tu kwamba wenzetu wa sehemu nyingine za nchi wanafaidi hela hizo. Ninaomba tusaidiwe kwani sisi pia ni Wakenya kama wengine,” akasema Bw Abala.

Kwa upande wake, Chifu wa Mararani, Ijuu Ware anaisifu serikali kuu kwa juhudi zake katika kupambana na wapiganaji wa Al-Shabaab na kuhakikisha usalama unadumishwa kwenye vijiji vyao.

Chifu wa Mararani, msituni Boni, Ijuu Ware. Anasema serikali kuu imetia bidhii kwa kudhibiti usalama ambao umekuwa ukitatizwa na wapiganaji wa Al-Shabaab kwenye vijiji vya Waboni. Aidha anaomba serikali kujikaza kusuluhisha matatizo ya kimsingi, ikiwemo miundomsingi ya elimu, barabara, vitambulisho, mawasiliano nakadhalika ili Waboni wajihisi kama wakenya wengine. PICHA | KALUME KAZUNGU

Awali, vijiji vya msitu wa Boni ambavyo ni Milimani, Basuba, Mararani, Mangai na Kiangwe, vilikuwa vikishuhudia mashambulio ya mara kwa mara kutoka kwa Al-Shabaab, hali iliyowasukuma wakazi kulala msituni kila usiku unapowadia.

Aidha serikali kuu ilizindua operesheni ya usalama kwa jina Linda Boni mnamo Septemba 2015, dhamira kuu ikiwa ni kuwasaka na kuwamaliza au kuwafurusha wapiganaji wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu wa Boni.

“Twashukuru. Tangu operesheni izinduliwe, usalama umeboreshwa na tunalala majumbani mwetu raha mstarehe, iwe ni usiku au mchana. Ombi letu ni shule zifunguliwe, hospitali na zahanati pia zijengwe kuhudumia wananchi wetu. Vijana hapa pia wapewe vitambulisho na matatizo mengine yasuluhishwe. Tukifanyiwa hayo tutajivunia kuwa wakenya zaidi,” akasema Bw Ware.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto awateua makatibu wawili wa wizara kujaza nafasi...

Madaraka Dei Juni 1, 2023

T L