• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 8:00 AM
‘Nabii Yohana wa Tano’ aitwa afike mbele ya polisi Juni 2

‘Nabii Yohana wa Tano’ aitwa afike mbele ya polisi Juni 2

NA JESSE CHENGE

IDARA ya polisi katika Kaunti ya Bungoma imemwagiza mhubiri Geoffrey Nakalira Wanyama, 83, almaarufu ‘Nabii Yohana wa Tano’ wa kanisa la Muungano Church for All Nations liloko Nandolia eneobunge la Kanduyi afike katika afisi ya kamanda wa polisi mnamo Juni 2, 2023 ili ahojiwe.

Kulingana na kamanda wa polisi Kauti ya Bungoma Francis Kooli, raia walitoa ombi kwa idara hiyo kumchunguza mhubiri huyo mwenye wake 42 na watoto 289 wakidai kwamba huenda anatumia nafasi hiyo kueneza itikadi kali.

Mhubiri Geoffrey Nakalira Wanyama (kushoto), 83, almaarufu ‘Nabii Yohana wa Tano’ wa kanisa la Muungano Church for All Nations akiwa na baadhi ya washirika. PICHA | JESSE CHENGE

‘Nabii Yohana wa Tano’ anakuwa wa pili kujipata pabaya katika eneo hilo baada ya Eliud Wekesa almaarufu ‘Yesu wa Tongaren’ kuhojiwa na hata kufikishwa mahakamani kabla ya kuachiliwa huru. Yesu wa Tongaren wa kanisa la New Jerusalem alitakiwa ajieleze namna alivyopata jina hilo Yesu huku pia akidaiwa kueneza itikadi kali. Upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha madai dhidi ya mhubiri huyo.

Naye ‘Nabii Yohana wa Tano’ amewashangaza wengi kwa kubuni ‘Biblia’ yake yenye vitabu 93 ambayo anatumia kuhubiri injili katika kanisa lake kinyume na wahubiri wengine ambao hutumia Biblia Takatifu yenye vitabu 66. Zaidi na hayo, ‘Nabii Yohana wa Tano’ pia amebuni ‘amri’ 12 badala ya amri 10 ambazo Musa alikabidhiwa katika Mlima wa Sinai.

Maafisa wa polisi wakiwa nyumbani kwake mhubiri Geoffrey Nakalira Wanyama, 83, almaarufu ‘Nabii Yohana wa Tano’ wa kanisa la Muungano Church for All Nations. PICHA | JESSE CHENGE

Maafisa wa polisi katika Kaunti ya Bungoma wamekuwa wakifanya msako wa makanisa ili kubaini iwapo wahubiri wamesajili madhehebu yao na kama wanahubiri wa injili wamekuwa wakizingatia sheria za nchi.

  • Tags

You can share this post!

Bellingham atawazwa Mchezaji Bora wa Bundesliga 2022-23

Tume ya Rais Ruto kuhusu uchunguzi Shakahola yazimwa na...

T L