• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Ndege mbili za helikopta zahusika katika ajali tofauti Wajir

Ndege mbili za helikopta zahusika katika ajali tofauti Wajir

Na MANASE OTSIALO

Takriban watu watatu wamejeruhiwa baada ya ndege aina ya helikopta kuanguka katika maeneo tofauti katika matukio yaliyoachana kwa masaa pekee Novemba 20, 2023.

Katika kisa cha kwanza, watu watatu wamethibitishwa kujeruhiwa baada ya helikopta ya kibinafsi kuanguka katika uwanja wa ndege wa Wajir.

Manusura hao walijumuisha rubani na maafisa wawili ambao walikuwa wanaenda kuchukua vifaa vya mtihani kutoka Arbajahan kuelekea Wajir mjini.

Katika kisa cha pili, helikopta ya kijeshi ambayo ilikuwa inasambaza chakula eneo la Buna, Wajir ilianguka muda mfupi baada ya kupaa.

Kulingana na video iliyonaswa na waliokuwemo, ndege hiyo inaonekana ikiondoka na sekunde chache baadaye inaonekana ikianguka na kuvunjika.

Msemaji wa Jeshi Kanali Zipporah Kioko alithibitisha tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa zaidi kadiri alivyozipata.

Akithibitisha kisa cha kwanza, Kamishna wa Kaskazini Mashariki John Otieno alisema ndege hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kupaa.

“Ndege hiyo ilikumbwa na matatizo ya kimitambo yaliyoisababisha kuanguka dakika kadhaa baaada ya kupaa na kujeruhi watu watatu,” alisema.

Chanzo cha kuanguka kwa helikopta hiyo yenye nambari ya usajili 5Y-SDL hakikubainika mara moja.

Alisema manusura hao walikimbizwa hospitalini.

Hali ya majeruhi haijulikani katika kisa cha pili kufikia wakati wa kuchapisha taarifa hii.

Hivi ni visa vya tatu kutokea chini ya wiki mbili.

Mnamo Novemba 9, marubani wawili wa jeshi walilazwa hospitalini baada ya ndege yao kuanguka katika eneo la Kisamis, Kajiado Magharibi.

Hii ilikuwa baada ya ndege ya Air Force kugonga waya angani ilipokuwa inapaa kuelekea Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Uchumi uko sawa mpuuzeni Raila, Ruto aambia Wakenya

ODM sasa yachakura mitandaoni ikisaka wafuasi wapya...

T L