• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Ndoa zasimama talaka zikipungua nchini, afichua Kadhi Mkuu

Ndoa zasimama talaka zikipungua nchini, afichua Kadhi Mkuu

NA KALUME KAZUNGU

TALAKA baina ya wanandoa wa dini ya Kiislamu kaunti ya Lamu, Pwani na Kenya kwa ujumla zimepungua kwa kiasi kikubwa.

Haya ni kulingana na Kadhi Mkuu nchini, Athman Abdulhalim Hussein aliyetaja kuwepo kwa asilimia karibu 20 pekee ya talaka ambazo zimerekodiwa na afisi yake kwa sasa.

Akizungumza wakati wa kongamano lililokutanisha afisi ya Kadhi Mkuu na wanawake wa Lamu mnamo Ijumaa, Bw Hussein alitaja ushirikiano uliopo kati ya mabaraza ya viongozi wa dini ya Kiislamu, jamii na idara ya Mahakama ya Kadhi nchini kuwa sababu muhimu za kupungua kwa visa vya talaka kati ya wanandoa Lamu na nchini kwa jumla.

Bw Hussein alitaja madai ya idadi ya talaka, hasa miongoni mwa wanandoa waislamu kwamba imeongezeka nchini kuwa dhana tu.

“Kusema kweli wanaodai kwamba kuna kesi nyingi za kutalakiana kati ya wanandoa waislamu naichukulia kuwa ni dhana tu. Ukweli ni kwamba kesi zimepungua pakubwa. Naweza sema kwa sasa tuko na asilimia 20 pekee. Bado ninahisi hiyo idadi yafaa kushughulikiwa vilivyo ili ipungue hata zaidi. Asilimia ndogo hiyo ya talaka inashuhudiwa kutokana nja ushirikiano wetu kama mahakama ya kadhi, viongozi wa dini na jamii,” akasema Bw Hussein.

Kadhi huyo mkuu aliwasisitizia wanandoa kudumisha upendo, maelewano, kuheshimiana na kuvumiliana ili kusaidia ndoa zisisambaratike, akitaja kuwa punde talaka inapofanyika wanaoumia mara nyingi huwa ni watoto.

Kadhalika aliwasisitizia wanawake wanaoolewa kuhakikisha wanakabidhiwa vyeti vya ndoa ili kusaidia wakati talaka zinapotokea.

“Utapata kwamba watu wameachana na hawana Cheti cha ndoa. Hilo tayari huwa ni tatizo linapokuja suala la urithi kwa mahakama zetu za kadhi.  Ni vyema mtu unapooa na kuolewa angalau mpate karatasi maalum mtakayotia sahihi kutambulisha kwamba ni kweli mumeoana. Kuweka wazi ni kwamba mahakama ya kadhi haitambui kamwe ndoa za siri. Lazima kuwe na thibitisho kwamba ni kweli mlioana rasmi,” akasema Bw Hussein.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK), tawi la Lamu Abubakar Shekuwe aliwapongeza wanawake wa Lamu kwa kuchangia pakubwa kupungua kwa talaka eneo hilo.

Kulingana na Bw Shekuwe, wanawake wa Lamu wamekuwa wakiwaelewa mabwana zao na pia kuzidisha upendo nyumbani na mahaba chumbani.

Alisema migogoro mingi inayoishia talaka miaka ya awali eneo hilo ilichangiwa na hulka ya wanandoa kukosa kuheshimiana na kudhalilishana, yamkini hata mbele ya watoto.

“Twafurahia kwamba hata Kadhi wetu Mkuu mwenyewe leo ametambua kwamba talaka zimepungua Lamu. Nachukua fursa hii kuwapongeza wanawake wetu. Hii inamaanisha nyinyi ni wenye mahaba tele kwa waume zenu nyumbani n ahata chumbani. Ninawashauri zaidi kwamba mwendelee na moyo huo huo. Sisi wanaume tuchanganyeni kabisa. Tumia mbinu zote kama mwanamke umnase mumeo ndipo hizi talaka tuzizike kwenye kaburi la sahau,” akasema Bw Shekuwe.

Kauli yake iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Kenya (SUPKEM), tawi la Lamu, Mohamed Abdulkadir aliyesisitiza haja ya wanandoa kuwa mstari wa mbele katika kudumisha heshima na maelewano na kuepuka kukimbilia kutafuta au kutoa talaka wakati migogoro inapozuka.

Wakati huo huo, Wanawake waislamu wa kisiwa cha Lamu wamemlilia Kadhi Mkuu, Athman Abdulhalim Hussein kuwasaidia kuhusiana na jinsi ndoa za siri zinavyowanyima haki ya urithi punde ndoa zinapoenda mafyongo.

Wakiongozwa na Msemaji wao Ummulkheir Ahmed, wanawake hao wamekiri kukithiri kwa idadi ya ndoa za siri eneo hilo.

Msemaji wa akina mama wakati wa kongamano kati yao na Kadhi Mkuu, Ummulkheir Ahmed. Amelia ndoa za siri zinanyima wanawake na watoto haki ya urithi wa mali talaka inapotolewa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Wanasema wengi wa wanawake walioolewa kwa siri huishia kuambulia patupu na watoto wao punde mume anapofariki au wakati talaka inapotolewa.

“Hapa Lamu ndoa za siri ni nyingi na hazina cheti chochote cha kuwatambulisha wanawake kwamba wameolewa na fulani.  Hili limewafanya wanawake wanakaa kwa muda na mwanamume kwa makubaliano ya muda kiasi kwamba wanazaa watoto na familia inapanuka. Kilio kinajiri punde kunapozuka mtafaruku unaoishia kwa talaka. Unapata kwamba mama anaachwa na watoto wake na hapati haki popote. Ningeomba afisi ya kadhi wetu mkuu kutusaidia ili wanawake wanaoolewa kwa siri wapate haki,” akasema Bi Ahmed.

Kongamano hilo la siku moja liliandaliwa kwenye ukumbi wa Lamu Fort na kufadhiliwa na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (MUHURI).

Mshirikishi wa MUHURI, tawi la Lamu, Mohamed Skanda akizungumza wakati wa kongamano la Kadhi Mkuu eneo la Lamu Fort mnamo Ijumaa, Septemba 15, 2023. PICHA | KALUME KAZUNGU

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mshirikishi wa MUHURI kaunti ya Lamu, Mohamed Skanda alieleza kutamaushwa kwake na jinsi talaka zinavyowasukuma vijana wengi kujiingiza kwa uhalifu na hata kuishia kushtakiwa, kuhukumiwa na kufungwa jela.

“Mbali na kuwa mshirikishi wa MUHURI, mimi pia ni mwanachama wa kamati ya Watumiaji wa Korti (CUC) hapa Lamu. Utapata kwamba kesi nyingi zinazowasilishwa mahakamani za uhalifu zinajumuisha vijana ambao wazazi wao waliachana. Kati ya watu watano wahalifu, utapata watatu ni wale wa mzazi mmoja baada ya wanandoa kutalikiana. Lazima tuheshimu ndoa na kupokea ushauri mwafaka utakaosaidia hizi talaka kusitishwa kwani madhara yake ni makubwa kwa watoto,” akasema Bw Skanda.

  • Tags

You can share this post!

Nauli nazo zapanda

RISASI YA SITA? Familia ya Raila yasisitiza hatastaafu siasa

T L