• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Ndoto ya BBI lazima itatimizwa, Uhuru asema

Ndoto ya BBI lazima itatimizwa, Uhuru asema

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta jana Jumapili alisema kuwa ndoto yake ya kubadilisha katiba ya Kenya iliyopitishwa 2010 kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), lazima itatimia japo mchakato huo ulisitishwa na Mahakama.

Akihutubu alipoongoza nchi kuadhimisha sherehe za 58 za Jamhuri Dei jijini Nairobi, Rais Kenyatta alisema BBI iliahirishwa tu na kwamba ni lazima mianya iliyo katika katiba itazibwa kupitia marekebisho.

“Haja ya kushirikiana na kuziba mwanya kwenye ukuta wa taifa letu kulisababisha umuhimu wa kuirekebisha Katiba yetu. Na ijapokuwa Mpango wa maridhiano wa BBI ulikumbwa na vikwazo vya kisheria, ninachoweza kusema tu ni kwamba ndoto ya BBI iliahirishwa. Siku moja, wakati mmoja, itafanyika kwa sababu nchi haiwezi kuhimili upendeleo wa kikabila na utengano kama vile ambavyo haiwezi kuhimili uwakilishi potofu usio wa haki. Hii ni kasoro ya kimuundo ambayo lazima tuirekebishe,” akasema Rais.

Alisema kwamba mchakato huo alioanzisha na Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ulichangiwa na haja ya kumaliza matatizo yanayosababishwa na nchi kugawanyika.

“Na wakati aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Raila Odinga na mimi tulipoazimia kushirikiana tarehe 8 Mwezi Machi mwaka 2018, ilikuwa ni kwa sababu tuliona mwanya kwenye ukuta wa taifa letu. Tulipitia chaguzi mbili ambazo ziliiletea nchi hasara ya Sh1 trilioni na tulikuwa tukiona taifa lenye mgawanyiko mkubwa. Kwa sababu tulikuwa tumetofautiana kwa heshima, tulijua hii ilikuwa hatua ya ufanisi. Ilikuwa vigumu, lakini muhimu, kutambua kwamba sisi kama Wakenya tunahitaji kila mmoja na taifa badala ya ubinafsi, jinsi baba zetu walivyokuwa wametufunza kushirikiana kuimarisha azma yetu,” alisema Rais Kenyatta.

You can share this post!

Hofu vimbunga vikiua watu 100

TAHARIRI: Hotuba ya Uhuru ichochee kuondoa ubaguzi na...

T L