• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 2:24 PM
‘Niko tayari kuwa rais wa muhula mmoja’

‘Niko tayari kuwa rais wa muhula mmoja’

Na ONYANGO K’ONYANGO

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amedokeza kuwa atahudumu muhula mmoja pekee akichaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Alisema kuwa alitangaza azma ya kuwania urais kutokana na ombi la wafuasi wake wakati wa mikutano ya Azimio la Umoja aliyofanya sehemu mbalimbali nchini.

Alifanya mikutano hiyo baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali Mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), Septemba 2021.

Kwenye mahojiano katika runinga moja Jumatano usiku, Bw Odinga alisema yu tayari kuhudumu kama rais kwa muhula mmoja kutokana na umri wake mkubwa.

“Ikiwa Wakenya ambao wameniomba niwanie urais kwa mara ya tano watataka nihudumu kwa miaka mitano pekee, nitakubali. Rais wa Amerika Joe Biden ni mkubwa kwangu kwa mwaka mmoja na anaongoza vizuri. Je, yeye pia anaweza kuulizwa swali kama hilo?” akauliza Bw Odinga.

Kauli ya Bw Odinga inajiri wakati ambapo wandani wa Rais Uhuru Kenyatta wakiongozwa na naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe wakifananisha urais wa kiongozi huyo wa ODM na ule wa aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela.

Bw Murathe alisema Waziri huyo Mkuu wa zamani anafaa “kutunukiwa” kiti hicho cha urais kutokana na juhudi zake za kupigania demokrasia nchini kwa miaka mingi.

“Tunaamini kuwa wakati umetimu kwa Wakenya kumzawidi Raila Amolo Odinga kwa miaka mingi ambayo amepigania utawala bora nchini. Yeye ni sawa na Mandela. Huu ni wakati wake. Na tunataka kumweleza Raila kwamba awe rais wa mpito ambaye atakuza kizazi kipya cha viongozi wachanga watakaochukua usukani 2027,” akasema.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi alisema kuacha kumbukumbu nzuri ya uongozi hakutegemei miaka ambayo kiongozi amehudumu.

Uamuzi

“Kwa hivyo, hata ikiwa Bw Odinga atahudumu kwa muhula mmoja, uamuzi huo ni wake. Nikimtathmini Raila kwa mtazamo wa kihistoria, nadhani yeye si kiongozi anayeongozwa na tamaa ya mamlaka na pesa. Anataka kuacha sifa na kumbukumbu. Kwa hivyo, ni yeye ataamua muda ambao utamwezesha kufikia lengo hilo,” akasema Bw Mbadi ambaye ni mbunge wa Suba Kusini.

Bw Odinga aliwania urais kwa mara ya kwanza mnamo 1997 kwa tiketi ya chama cha National Development Party (NDP) na kuwa nambari tatu katika uchaguzi ambapo rais wa zamani marehemu Daniel Moi alishinda.

Rais mstaafu Mwai Kibaki alikuwa wa pili katika kinyang’anyiro hicho kilichoshirikisha wagombeaji wanane.

Mnamo 2002, Bw Odinga aliungana na makamu wa rais wa zamani marehemu Wamalwa Kijana, kiongozi wa Narc Charity Ngilu na baadhi ya viongozi wa Kanu na kumpiga jeki Bw Kibaki akashida urais.

Ushindi huo ulifikiwa chini ya mwavuli wa muungano huo wa Narc.

Bw Odinga aliwania urais mara ya pili mnamo 2007 kwa tiketi ya chama cha ODM na kuibuka wa pili nyuma ya Bw Kibaki aliyetetea kiti chake kwa tiketi ya chama cha Party of National Unity (PNU).

Aliwania tena katika chaguzi za 2013 na 2017 na kushindwa na Rais wa sasa Uhuru Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

Azimio la Raila lamtikisa Ruto

Mihadarati: Magoha aunga wanafunzi wapimwe

T L