NA RICHARD MUNGUTI
SENETA wa Busia Okiya Omtatah ameanza mchakato wa kuokoa wananchi kwa kupeleka kesi katika Mahakama Kuu akiomba vipengee tata 13 kwenye Mswada wa Fedha wa 2023 vinavyowalazimisha wananchi kulipa madeni, ada na ushuru vifutiliwe mbali.
Bw Omtatah amesema kupitishwa na kuidhinishwa kwa mswada huo na Rais William Ruto kutakuwa kumeipa serikali idhini ya kuwatoza wananchi ada na ushuru kwa nguvu, jambo analosema ni kinyume cha sheria.
Anaomba Mahakama Kuu iharamishe mswada huo na kutoa hukumu kwamba hatua hiyo ya kuwashurutisha wananchi kulipa kodi na ada ya nyumba ni unyanyasaji wa hali ya juu.
Seneta huyo ambaye hivi majuzi alimweleza Rais Ruto angewasilisha kesi kupinga mswada huo wa fedha alipozuru Kaunti ya Busia, amedokeza ushuru wanaotozwa wananchi unatumika kulipa mikopo ambayo watu binafsi walielekeza kwa akaunti zao kujinufaisha walipokuwa serikalini.
Bw Omtatah ameeleza kinanga ubaga kwamba wananchi wamebebeshwa mzigo mzito wa kulipa madeni ambayo “pesa zenyewe hazikutumika kustawisha nchi hii.”
Seneta huyo anahoji madeni ambayo nchi inadaiwa akisema “baadhi ya madeni haya ni mikopo ya watu binafsi waliobwaga kwa wananchi.”
Amefafanua kwamba Rais Ruto ameagiza watumishi wa umma wakatwe ada ya asilimia tatu ya mapato yao kuekeza katika miradi ya nyumba.
Bw Omtatah amesema hakuna sheria inayomlazimisha mtumishi wa umma au mwananchi yeyote kuweka hazina.
“Hakuna sheria inayomlazimisha mfanyakazi wa umma kujiwekea hazina,” Bw Omtata anasema katika kesi hiyo aliyowashtaki Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Waziri wa Fedha na Mwanasheria Mkuu.
Seneta huyo amechambua mswada huo na kusema katika kipindi cha miaka saba kila mtumishi wa umma atakuwa amekatwa Sh420,000.
“Sh420,000 haziwezi zikajenga nyumba ya wastani,” Bw Omtatah akasema.
Hivyo basi, Omtata amesema Mswada wa Fedha wa 2023 ambao umewasilishwa katila Bunge la Kitaifa hauzingatii kamwe maslahi ya wananchi wa kawaida.
Ili kuwaokoa wananchi, Bw Omtatah amevitambua na kuvifafanua vipengee tata anavyosema viking’olewa, wananchi watapata afueni.
Vipengee ambavyo Bw Omtatah amevitambua vinakandamiza wananchi ni nambari 28, 30, 33, 34, 36, 52, 56, 59, 73, 74, 76, 78, na 79 katika Mswada wa Fedha, 2023.
Anaomba Mahakama Kuu itathmini kwa undani zaidi vipengee hivi anavyosema vinashurutisha wananchi kulipa ushuru utakaotumika kulipa madeni ambayo kiwango chake alisema hakijulikani.
Basi, seneta Omtatah ameomba Mahakama Kuu ishurutishe Serikali kutangaza deni kamili ambalo nchi inadaiwa na mataifa ya kigeni na kwamba likaguliwe.
Bw Omtatah anadai serikali imeongezea kiwango cha deni hili kwa Sh3.7 trilioni.
“Kiwango cha deni kinachotangazwa kila mara ni Sh8.7 trilioni lakini hesabu kamili haijulikani japo ni kama takriban Sh4.7 trilioni. Wananchi wameongezewa kiwango cha deni kwa zaidi ya Sh3.7 trilioni,” Bw Omtatah akafichua alipozugumza na wanahabari katika Mahakama Kuu ya Milimani.
Akipinga kupitishwa kwa mswada huo na Bunge la Kitaifa Bw Omtatah ameeleza mahakama kwamba Rais William Ruto alinyakua mamlaka ya utozaji ushuru badala ya Bunge la Kitaifa na Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA).
Seneta huyo wa Busia amesema mswada huo unalenga kuwakandamiza wananchi kwa kuwatoza kodi kinyuma cha sheria.
Ameomba kesi hiyo iratibiwe kuwa ya dharura kisha ipelekwe kwa Jaji Mkuu Martha Koome ateue majaji wasiopungua watatu kuisikiliza na kuamua.
“Naomba kesi hii iratibiwe kuwa ya dharura kisha ipelekwe kwa Jaji Koome kuteua jopo la majaji wasiopungua watatu kuisikiliza na kuamua kwa vile kuruhusu wananchi walipe ushuru kinyume cha sheria ni kuwaibia,” Bw Omtatah akasema katika kesi aliyoshtaki Ijumaa, Juni 2, 2023.
Seneta Omtatah amesema endapo bunge litapitisha mswada huo litakuwa limewakandamiza wananchi.
Bw Omtatah amesema Rais Ruto anatumia vibaya Idara ya Mahakama, Bunge na Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru nchini (KRA) katika harakati zake za kutafuta pesa za kuendeleza nchi.
Kesi hiyo itawasilishwa kwa Jaji wa Mahakama ya Milimani mnamo Juni 5, 2023 kwa maagizo zaidi.