• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Pasta tapeli wa mashamba taabani

Pasta tapeli wa mashamba taabani

Na RICHARD MUNGUTI

PASTA wa Kanisa la Kipendekoste ameshtakiwa kwa kupeli Wakenya watatu wanaoishi Amerika Sh6.8 milioni akidai atawanunulia mashamba jijini Nairobi.

Pasta Catherine Wairimu Ng’ang’a wa Arise and Healing and Deliverance Church lililoko eneo la Githurai ameshtakiwa katika Mahakama ya Milimani.

Aliposomewa mashtaka manne mbele ya Hakimu Mwandamizi Bi Zainab Abdul Pasta Wairimu alikana kuwalaghai walalamishi hao.

Upande wa mashtaka ulisema mhubiri huyu mwenye umri wa miaka 53 aliwafuja dada wawili Noel Njeri Ngure na Lilian Muthoni Ngure pamoja na Anne Nyambura Njogu Sh6, 870, 000 akidai atawanunulia mashamba katika eneo la Mowlem Naironi.

Alishtakiwa kwamba alipokea pesa hizo kati ya Februari na Septemba 2021.

Hakimu alifahamishwa kuwa Pasta Wairimu alipokea Sh4 milioni kutoka kwa Noel akidai atamuuzia ploti nambari Mowlem/Nairobi Block 169/285 ilhali alijua alikuwa anadanganya.

Mshtakiwa alitiwa nguvuni Mei 28, 2023 na kuzuiliwa hadi Jumatatu, Mei 29, 2023 alipofikishwa kortini.

Alikana kupokea Sh1, 735, 000 kutoka kwa Lilian Muthoni Ngure akidai atamuuzia ploti Mowlem/Nairobi Block 169/287.

Shtaka la tatu lilisema alipokea kitita cha Sh900, 000 kutoka kwa Lilian Muthoni Ngure kati ya Agosti 31 na Septemba 24, 2021 wakati huu akidai atamuuzia maduka matatu katika soko la New Wakulima Kangundo Road.

Pasta huyo alishtakiwa kumpora Ann Nyambura Njogu Sh253, 200 akidai alikuwa na uwezo wa kumuuzia ploti nambari Mowlem/Nairobi Block 169/286.

Aliomba aachiliwe kwa dhamana.

Bi Abdul alimwamuru alipe dhamana ya Sh500, 000.

 

 

  • Tags

You can share this post!

JIPENDE: Tabia zinazoonyesha mja hajiamini

Mhubiri kutoka Nigeria ashtakiwa kwa kupora benki mamilioni...

T L