• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Pigo kuu Pasta Ezekiel akizuiwa kuhudhuria mkutano wa injili

Pigo kuu Pasta Ezekiel akizuiwa kuhudhuria mkutano wa injili

NA WINNIE ATIENO

MHUBURI matata Ezekiel Odero anayekabiliwa na mashtaka mahakamani kwa shutuma za mauaji, utakatishaji wa pesa, kusaidia mtu kujitoa uhai, utekaji nyara, mafunzo ya itikadi kali ya kidini, unyanyasaji wa watoto na ufisadi alipata pigo kubwa baada ya polisi kumzuia kuhudhuria mkutano wa kidini.

Mhubiri huyo maarufu alikuwa amepania kusafiri kutoka kanisa lake la Mavueni hadi Machakos kwa mkutano wa injili hii leo, Jumapili, Juni 4, 2023 kupitia mwaliko wa Askofu Pius Muiru mwanzilishi wa Maximum Miracle Centre, lakini alizuiliwa baada ya kibali kufutiliwa mbali.

Bw Muiru alisema alikuwa amepewa kibali cha kuandaa mkutano wake wa kidini lakini alipoanza kutangaza hadharani kuwa mwandani wake Bw Ezekiel atahudhuria alipokonywa kibali.

Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, Mhubiri Muiru alisema wamepata hasara baada ya serikali kupiga marufuku mkutano wake akiutaja uamuzi huo kuwa maonevu na ukiukaji wa Katiba ya uhuru wa kuabudu.

Hata hivyo, polisi walithibitisha kuwa kibali hicho kimefutiliwa mbali kufuatia kesi zinazomkabili mahakamani.

“Kamati ya usalama ya kaunti iliamuru kuwa Bw Ezekiel hafai kuhudhuria mkutano wa injili sababu ya kesi anazokabiliwa nazo mahakamani,” alisema afisa mmoja huko Machakos akiomba jina lake libanwe.

Bw Muiru alisema alimwalika mhubiri mwenzake ambaye wamejuana kwa zaidi ya miaka 10.

“Tulikuwa tumetumia pesa nyingi kwa matangazo ikiwemo hata wageni wetu ambao walikuwa wamekodi hoteli. Ni kisa sawia na kile kilichomkumba Bw Ezekiel nchini Dodoma ambapo alikuwa ameandaa mkutano huo wa injili badala yake akashikwa nchini Kenya kabla aondoke kuelekea Tanzania na kulala korokoroni,” alisema Bw Muiru.

Mawakili wa mhubiri Ezekiel akiongozwa na Bw Danstan Omari, Bw Cliff Ombeta, Bw Duncan Osoro na Bw Sam Nyaberi waliishtumu serikali kwa kumzuia kuhudhuria mkutano wa Bw Muiru wakisema ni ukiukaji wa Katiba ambayo inampa mamlaka ya uhuru wa kuabudu.

“Pasta Ezekiel amepata hasara ya zaidi ya Sh500, 000 ikiwemo kukodisha hema, magari ya kupaza sauti, kuchapisha habari kuhusu mkutano huo ikiwemo malipo mengine. Lakini hasara kubwa imetoka kwa waumini ambao wamekosa chakula cha roho,” alisema Bw Omari.

Alisema mteja wake atafikishwa katika idara ya uhalifu na uchunguzi makosa ya jinai katika makao makuu ya polisi eneo la Pwani hapo kesho (Jumatatu) kuhojiwa kulingana na maagizo ya mahakama.

Hata hivyo, alisema Bw Ezekiel amewasamehe wale wote ambao wanamhukumu.

Bw Ombeta alisema Pasta Ezekiel atapiga kambi jijini Nairobi wiki ijayo kuandaa mkutano mwingine.

“Tofauti na Machakos, hapa tunataka Bw Ezekiel aende akaombe idhini akitumia jina lake ndio tuone kama atanyimwa au atapewa tujue panapovuja. Mteja wetu anapigwa vita kila kuchao, inasikitisha sana, lakini anapata motisha,” aliongeza wakili huyo.

Alisema masaibu anayokumbana nayo ni mapito.

 

  • Tags

You can share this post!

Ulinzi Starlets mbioni kutetea ubingwa wa Kombe la FKF

Musalia afunika Gachagua

T L