• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:30 PM
Polisi watwaa vifaa vya kanisa la Ezekiel Odero

Polisi watwaa vifaa vya kanisa la Ezekiel Odero

Na JURGEN NAMBEKA

POLISI wa kupambana na ugaidi (ATPU) waliingilia kanisa la mhubiri Ezekiel Odero na kutwaa vifaa vyake vya mawasiliano, hifadhi za data za kompyuta, maji ya uzima na vitambaa katika kanisa la New Life Center.

Kulingana na mawakili wake Cliff Ombeta na Danstan Omari, polisi hao walidai kuchukua na kuzuilia vifaa hivyo kwa ajili ya uchunguzi.

Bw Danstan Omari ameeleza kuwa masaibu ya mhubiri huyo yamezidi kuwa mengi, baada ya msajili wa mashirika kutoa ilani ya kutaka kufutilia mbali usajili wa kanisa hilo kwa madai ya kutolipa kodi.

“Polisi hao walikuja kwa kanisa Jumanne na kuchukua vifaa hivyo wakidai kuwa walikuwa wakivipeleka kwa uchunguzi zaidi,” alisema Bw Ombeta wakizungumza na wanahabari katika hoteli ya Sarova whitesands jijini Mombasa.

Mhubiri huyo alikuwa akichunguzwa kwa madai ya kuhusishwa na mhubiri tata Paul Mackenzie na mauaji ya Shakahola.Hata hivyo, Bw Odero amejitenga na Bw Mackenzie wa kanisa la Good News International Church.Bw Omari alieleza kuwa wangeelekea mahakamani kumshtaki Msajili wa mashirika pamoja na afisi yake kwa njama ya kuficha faili ya kanisa hilo.

Isitoshe walidai kuwa wangeishtaki afisi hiyo kwa matumizi mabaya ya mamlaka yake.

“Kuna njama ya kumhangaisha Bw Odero na kanisa lake. Shirika la kukusanya kodi (KRA) lilisema kanisa limekuwa likifuata sheria. Msajili wa mashirika anaeleza kuwa kanisa halijakuwa likilipia kodi tuwasilishe stakabadhi za mapato kwa KRA. Tutaelekea mahakamani,” akasema Bw Omari.Wawili hao walieleza kuwa mengi yanayomsibu mhubiri huyo ni ya kumfedheheshwa yeye na huduma yake kwa kua na zaidi ya waumini milioni 10.

Kando na hilo, walieleza kuwa serikali imekuwa ikichunguza tetesi za ardhi la kanisa inayomilikiwa na kanisa hilo kupatikana kwa njia isiyo halali, licha ya Tume ya ardhi (NLC) kueleza kuwa vyeti vya ardhi hiyo vilikuwa halali.

“NLC imeeleza kuwa ardhi zimesajiliwa kihalali. Sielewi mbona msajili wa mashirika anatupeleka huku na kule na kuficha faili ya kanisa,” akasema Bw Ombeta.

Aidha, walihoji kuwa faili hiyo ambayo kwa sasa inadaiwa kupotea, imewazuilia wao kuwasilisha stakabadhi za mapato ya kanisa hilo kwa KRA.

Mawakili hao walilalamika kuwa msajili wa mashirika alikuwa ametoa ilani ya kufutilia mbali usajili wa kanisa hilo siku 21, kanisa halijapata ilani hiyo ila walipata taarifa hizo kupitia kwa vyombo vya habari.

Kanisa hilo lilisajiliwa mnamo 2012 kwa mujibu wao, na haiwezekani kuwa madai haya yote yanajitokeza wakati huu.

“Madai yanayojitokeza sasa hivi hayana msingi. Kuna watu walioingiwa na wivu kwa kuwa mhubiri huyo ana wafuasi wengi wanaoweza kujaza uwanja. Walifunga stesheni ya televisheni kwa muda, mahakama ikafungua. Mara akaunti za benki zikafungwa. Haya yote ni ya kuwahangaisha waumini wake milioni 10,” akasema Bw Omari.

 

  • Tags

You can share this post!

Polisi wapata viungo zaidi vya mwanamume

Soko la utalii lapigwa jeki kutokana na wawekezaji wa...

T L