• Nairobi
  • Last Updated December 3rd, 2023 7:00 PM
Programu ya kutatua migogoro kidijitali yazinduliwa nchini

Programu ya kutatua migogoro kidijitali yazinduliwa nchini

NA FARHIYA HUSSEIN

PROGRAMU ya kidijitali iliyoundwa kutatua mizozo ya mtandaoni baina ya watumiaji wa mitandao ya kijamii, imezinduliwa nchini.

Kenya inakuwa taifa la tatu kukumbatia teknolojia hii baada ya Sri Lanka na Nigeria.

Uzinduzi huo ni sehemu ya mpango wa kimataifa unaoongozwa na Search for Common Ground (SFCG), shirika la kimataifa lisilo la kiserikali ambalo linafanya kazi kukomesha migogoro ya vurugu na kukuza jamii za haki.

Kulingana na shirika hilo, ni kwamba wakuu wake walitambua hitaji kubwa la mipango ya kidijitali ya kutumika kupalilia amani miongoni mwa wanajamii, haswa katika maeneo ambayo yalikuwa na viwango vya juu vya migogoro.

SFCG ilibaini mitandao ya kijamii kuwa jukwaa lenye mawasiliano lakini pia mitandao hiyo imekuwa chanzo cha mafarakano na uenezaji wa dhana potovu.

Hii ndio maana kwamba kwa ushirikiano na wataalamu, watafiti, wasomi, mashirika yanayoongozwa na vijana na mashirika ya kiraia, wameibuka na teknolojia inayosaidia kutatua suala hili.

Lengo kuu la SFCG na washirika wengine ni kuhimiza watumiaji wa mitandao ya kijamii kufikiria tofauti kuhusu jinsi wanavyoweza kutatua mizozo mtandaoni.

Mbinu yao ilihusisha kuwapa watu ujuzi muhimu na mitazamo kuhusu utambulisho, mtazamo, na mawasiliano yasiyo ya vurugu.

Chombo hicho, BridgeBot, kinapatikana kwenye jukwaa la WhatsApp. BridgeBot iliundwa kwa ushirikiano na TangibleAI, kampuni inayoongoza ya maendeleo ya kiteknolojia.

“Msukumo wa kubuni BridgeBot ulitokana na utafiti wa kina ambao ulifichua mtindo ulioonyesha kwamba wakati majadiliano ya mtandaoni yanapopamba moto, baadhi ya watu hujiondoa kwenye mazungumzo au wanajibu kwa njia inayoleta chuki,” Mkurugenzi wa SFCG Nchini Kenya na Somalia Bi Judy Kimamo alisema.

Bi Kimamo alitambua zaidi udharura wa kushughulikia suala hili.

“Kutoelewana mtandaoni kunaweza kuchangia vurugu na kugawanya zaidi jamii. Lengo letu ni kuunda jukwaa la kidijitali ambalo litawawezesha watu kujifunza kuwasiliana kwa ufanisi zaidi, hata kukiwa na maono au mtazamo kinzani,” akasema.

Kabla ya uzinduzi, BridgeBot, ilikuwa imefanyiwa majaribio makali kwa zaidi ya miezi saba katika nchi zilizochaguliwa kote ulimwenguni. Iliendelea kubadilika kulingana na mwingiliano wa watumiaji na maoni ya watumiaji.

Bi Kimamo alisema BridgeBot sio tu njia ya mapatanisho katika mitandao ya kijamii lakini pia itasaidia kushauri na kuwaelekeza watumiaji kutatua mgogoro wa mtandaoni kwa njia inayofaa.

Mkazi wa Mombasa mwenye ujuzi wa teknolojia, Bw Martin Owino, alisema alikumbatia chombo hicho kama njia ya kuziba pengo kati ya mitazamo inayokinzana na kukuza utamaduni wa mazungumzo ya amani mtandaoni.

Mmoja wa watumiaji wa BridgeBot, Bw Erick Agwanda, alielezea uzoefu wake, “Nilikuwa nikiepuka mijadala ya mtandaoni kwa sababu kila mara iligeuka kuwa mibaya. Lakini kupitia BridgeBot, nimejifunza kushiriki mijadala kwa njia inayofaa. Sio kubadilisha mawazo ya mtu, lakini kuelewa mtazamo wao.”

Inatarajiwa kuzinduliwa nchini Jordan na Lebanon pia.

  • Tags

You can share this post!

Bei ya pombe kuongezeka kwa asilimia 300 pendekezo la...

Vibanda vya mahasla kujitafutia riziki vyabomolewa South B

T L