• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Raila achemkia Serikali kufuatia kukamatwa kwa Msimamizi wa Bajeti

Raila achemkia Serikali kufuatia kukamatwa kwa Msimamizi wa Bajeti

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga ameikashifu serikali kufuatia kukamatwa na kushtakiwa kwa Msimamizi wa Bajeti (CoB) Margaret Nyakang’o kwa tuhuma za ulaghai.

Kwenye taarifa Jumanne Desemba 5, 2023, Bw Odinga amedai kuwa masaibu ya Dkt Nyakang’o yamechochewa na kujitolea kwake kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kitaalum na kufichua ufisadi serikalini.

“Sawa na Wakenya wengine, kukamatwa kwa msimamizi wa bajeti sio jambo la kushangaza kwa sababu dalili zake zilionekana. Hii ni kutokana na kujitolea kwake kufanya kazi kwa uadilifu katika utawala uliojaa wafisadi na wahalifu wa aina mbalimbali,” akasema.

“Tulijua wanapanga kumwelekea makosa yasiyo na msingi wowote ili wamwondoe afisini ili kutoa nafasi kwa mtu ambaye atafumbia macho uporaji unaondelea serikalini wakati huu,” Bw Odinga akaongeza.

Kiongozi huyo wa Azimio alisema kama chama watasimama na Dkt Nyakang’o na kumpa usaidizi wowote wanaoweza kwa ajili ya kupiga jeki vita dhidi ya ufisadi nchini.

Msimamizi huyo wa bajeti alikamatwa mjini Mombasa Jumanne asubuhi na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumlaghai Bi Claudia Mueni Sh29 milioni mnamo 2016. Aidha, alikabiliwa na mashtaka ya kuendesha shirika la akiba na mikopo (Sacco) bila leseni na kughushi stakabadhi.

Alikana makosa hayo na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh2 milioni au Sh500, 000 pesa taslimu. Kesi hiyo itatajwa Desemba 13, 2023.

 

  • Tags

You can share this post!

Mkenya aanza kutembea kilomita 500 kuchangisha pesa za...

Kuna ubaguzi katika misaada ya El Nino, mbunge Mishi Mboko...

T L