RICHARD MUNGUTI Na ALEX KALAMA
RAIS William Ruto jana Jumatatu alipata pigo baada ya mahakama kupiga breki tume yake aliyoteua kuchunguza vifo vya mamia ya watu katika shamba la Mhubiri Paul Mackenzi msituni Shakahola, Kaunti ya Kilifi.
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jessie Lesiit imeagizwa na Jaji Lawrence Mugambi isitishe mara moja uchunguzi huo hadi pale kesi iliyowasilishwa na kinara wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga itakaposikizwa na kuamuliwa.
Akisitisha utendakazi wa tume hiyo, Jaji Mugambi alisema asasi nyingine za serikali zinazojumuisha polisi, kamati ya Seneti inayoongozwa na Seneta wa Tana River Danson Mungatana na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu (KNCHR) zinachunguza vifo vya wafuasi wa Pasta Mackenzie walioshawishiwa kukataa kula na kunywa hadi kifo ili wakutane na Yesu.
Akasema Jaji Mugambi: “Kamati hizi zote zinatumia pesa za umma na vilevile jopo la Jaji Lesiit litakuwa linatumia pesa za umma. Huu utakuwa ni uharibifu mkubwa wa pesa za umma.”
Pia Jaji Mugambi alisema Rais Ruto aliteua tume hiyo kinyume cha sheria bila kushauriana na Jaji Mkuu Martha Koome.
Bw Odinga kupitia kwa wakili Paul Mwangi, alipinga uteuzi huo akisema kuwa Rais Ruto hakushauriana na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC). Azimio pia ilimkosoa Rais Ruto kwa kukaidi Katiba kwa kujitwika mamlaka asiyokuwa nayo.
Bw Odinga alieleza mahakama kuwa hatua hiyo ya Rais Ruto ya kuteua majaji kuongoza majopo ni kuingilia na kuvuruga uhuru wa utendakazi wa Idara ya Mahakama ambayo ni huru.
“Uteuzi wa tume hiyo unakinzana na katiba kwa kuwa sasa Rais Ruto na marais watakaomfuata watakuwa na tabia ya kuwashawishi majaji kwa kuwapa kazi kubwa na pesa nono kutekeleza utendakazi wao na kuwafanya kutoa maamuzi yanayoegemea upande mmoja,” Mwangi alifafanua akiomba tume hiyo ivunjiliwe mbali.
Azimio iliomba mahakama iagize kwamba hatua hiyo ya Rais Ruto ilikinzana na Katiba. Jaji huyo alisema, atakosea endapo ataruhusu tume hiyo ya Jaji Lesiit kuanza kazi kabla ya kesi inayoipinga kusikizwa na kuamuliwa.
Rais Ruto aliteua jopo hilo la wanachama wanane mnamo Mei 4,2023 kuchunguza mauaji ya halaiki ya wafuasi wa kanisa la Pasta Mackenzie. Pia tume hiyo ilitwikwa jukumu la kuchunguza baadhi ya makanisa na viongozi wao na kutoa mapendekezo ya kuwachuja mapasta wasiohitimu.
Mbali na kuchunguza vifo hivyo vya kushtusha, jopo la Jaji Lesiit lilipewa jukumu la kuchunguza dhuluma wanazofanyiwa waathiriwa ambao walikuwa waumini wa kanisa la Good News International la Mackenzie lililoko Kilifi.
Akisitisha shughuli hiyo, Jaji Mugambi alisema tume ya KNCHR ilieleza nia ya kujiunga na kesi iliyowasilishwa na Bw Odinga, ikidai, Rais Ruto hana mamlaka ya kubuni jopo la kuchunguza visa vya ukiukaji wa haki za binadamu.
Wakili wa Serikali, Emmanuel Mbita alipinga kesi hiyo ya Bw Odinga akimtetea Rais Ruto kwa kusema “hakukiuka sheria kwa kubuni tume hiyo kwa kuwa jukumu lake kuu ni kulinda haki za kila Mkenya”.
Pia alisema tume hiyo imepewa mamlaka kisheria kuchunguza na kutoa ripoti kuhusu athari za makanisa yanayohubiri injili yenye itikadi kali.
Bw Mbita alieleza Jaji Mugambi kuwa kuzima tume ya Jaji Lesiit ni kuwanyima haki waathiriwa na Wakenya wanaotapeliwa na mapasta kwa mafundisho potovu.
Jaji Lesiit aliteuliwa pamoja na wanachama Jaji (mstaafu) Mary Kasango, Eric Gumbo, Askofu Catherine Mutua, Jonathan Lodompui, Dkt Frank Njenga, Wanyama Musiambu na Albert Musasia.
Wakili Kioko Kilukumi aliteuliwa kuwa kiongozi wa kuwasilisha ushahidi katika tume hiyo. Bw Mbita aliomba mahakama itupilie mbali kesi hiyo ya Azimio. Jaji Mugambi alisema Azimio imezua masuala yaliyo na mashiko kisheria kuwezesha mahakama kuyaamua.