• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
Raila azindua safari ya ikulu kwa ahadi nyingi

Raila azindua safari ya ikulu kwa ahadi nyingi

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, jana alianza rasmi safari yake ya kuelekea Ikulu 2022, huku akipata uungwaji mkono kutoka kwa makundi mbalimbali.

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake waliojitokeza katika Uwanja wa Michezo wa Kasarani, jijini Nairobi kwa mkutano wa ‘Azimio la Umoja’, Bw Odinga pia alitoa msururu wa ahadi ambazo atatimizia Wakenya endapo atachaguliwa rais mwaka ujao.

Baadhi ya ahadi hizo ni kubuni nafasi za ajira kwa vijana, kuboresha sekta ya afya, elimu bora kwa wote, kuboresha maslahi ya wanawake, kubuni mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, kubuni mipango ya kushughulikia makundi yaliyotengwa katika jamii, kulinda na kuboresha mfumo wa ugatuzi, kuendeleza miradi iliyoanzishwa na tawala za hapo awali kati nyingine.

“Ninafahamu nitakuwa na mzigo mzito kutimiza ahadi ambazo nimetoa kwa Wakenya wote. Hata hivyo, naamini itakuwa safari yetu sisi sote ili kutimiza malengo yetu,” akasema Bw Odinga. Kiongozi huyo pia aligeuza mpango wa Azimio la Umoja kuwa vuguguvu la kisiasa, akisema lengo lake ni kuwashirikisha Wakenya wote kwenye safari yake.

Jumla ya magavana 31 na wabunge zaidi ya 50 kutoka vyama mbalimbali kama ODM, Jubilee, Kanu kati ya vingine walihudhuria hafla hiyo. Mawaziri kadhaa wakiwemo Peter Munya (Kilimo), Joe Mucheru (ICT), Sicily Kariuki (Maji) kati ya wengine walihudhuria, hali iliyoashiria mkono wa serikali kwenye hafla hiyo.

Ingawa Rais Uhuru Kenyatta hakuhudhuria hafla hiyo, wadadisi wanasema uwepo wa mawaziri hao unaonyesha walikuwa na “baraka” kutoka kwa Rais, ambaye yuko ziarani nchini Tanzania.Bw Odinga amekuwa akionekana kama “mradi wa kisiasa” wa serikali ya Rais Kenyatta 2022, baada ya kutofautiana na na Naibu Rais William Ruto.

Mkewe Bw Odinga, Bi Idah Odinga, alitangaza “kumwachilia” kigogo huyo kwa Wakenya, akisema yuko huru kuzuru sehemu mbalimbali nchini kutafuta uungwaji mkono kuwa rais wa tano.Baadhi ya makundi yaliyotangaza kuunga mkono azma yake ni mawaziri, magavana, wanawake, wabunge, walemavu, vijana, wafanyabiashara.

Wawakilishi wa makundi hayo walisema Bw Odinga ndiye kiongozi bora wanayeamini ataendeleza, kulinda na kutimiza matakwa yao. Jumatano, Bw Munya alisoma maamuzi ya mabwanyenye wa Mlima Kenya waliofanya kikao katika hoteli moja, Nairobi, kumwidhinisha Bw Odinga kama mgombea urais watakayemuunga mkono 2022.

“Kama magavana wa kutoka Mlima Kenya, tunakuunga mkono kwani tunahisi wewe ndiye kiongozi ambaye tutakuwa salama chini ya uongozi wake,” akasema Gavana Lee Kinyanjui (Nakuru), ambaye ni miongoni mwa magavana ambao wamekuwa wakimpigia debe Bw Odinga. Akizungumza kwa niaba ya wanawake, Gavana Charity Ngilu (Kitui) pia alitoa kauli kama hiyo.

“Tunajua tutakuwa chini ya kiongozi muungwana wakati utachukua uongozi wa nchi hii kama rais wa tano. Kama wanawake, tutakuunga mkono. Tunakuomba utumie utaalamu wako wa uhandisi kuboresha uchumi wa nchi hii,” akasema Bi Ngilu.

Barobaro Fikirini Jacobs na mwanadada Hezena Lemaletian, ambao walizungumza kwa niaba ya vijana, walisema hawatakubali kuwa chini ya wanasiasa wanaoeneza chuki na ukabila. Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Kitaifa cha Wafanyabiashara Kenya (KNCCI) na sekta ya kibinafsi, mwakilishi wa kundi hilo, Bw Richard Ngatia, alisema wana matumaini Bw Odinga atawashirikisha vilivyo kwenye serikali yake ikiwa atatwaa urais.

Bwanyenye SK Macharia alimtaja Bw Odinga kama kiongozi ambaye ameonyesha kujitolea kwake kupigania ukombozi wa Kenya, baada ya kufungwa gerezani kwa miaka minane wakati wa utawala wa Kanu.“Kilicho dhahiri ni kuwa, Bw Odinga ni kiongozi ambaye ana historia ya kuonyesha uzalendo wake kwa nchi.

Ameteseka sana pamoja na familia yake akipigania uwepo wa utawala bora nchini,” akasema Bw Macharia, aliyezungumza kwa niaba ya Wakfu wa Mlima Kenya (MKF). Uungwaji mkono huo unaonekana kuwa hatua kubwa kwa Bw Odinga, ambaye alitangaza rasmi nia yake kuwania urais jana.

You can share this post!

Korti ya Juu yashikilia uamuzi kuhusu jinsia

Wasimamizi waelezea hatua ilizopiga MKU katika utoaji...

T L