• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Reuben Kigame aitaka Azimio isitishe vitisho kugawa nchi

Reuben Kigame aitaka Azimio isitishe vitisho kugawa nchi

NA TITUS OMINDE

ALIYEKUWA mgombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 Reuben Kigame ametaka kiongozi wa Azimio la Umoja – One Kenya Raila odinga kuachana na ajenda ya kugawanya nchi ya Kenya.

Akihutubu mjini Eldoret, Bw Kigame alisema njia bora ya kuleta mabadiliko nchini na uongozi bora si kutaka kugawa nchi kama alivyotishia Bw Odinga.

Kigame alisema licha ya kuwa anaunga mkono Wakenya ambao wanapinga mswada wa kutozwa ushuru wa nyumba walakini si vyema kutumia suala hilo kutishia kugawanya taifa la Kenya kuwa mataifa mawili.

Kiongozi huyo alionya mipango kama hiyo ina uwezo mkubwa kusababisha umwagikaji wa damu nchini.

“Vitisho vya Azimio kuhusu kugawanya nchi yetu ni hatari kwa usalama wa taifa hili. Tabia kama hiyo inaweza ikafanya taifa la Kenya kuwa kama mataifa mengine barani ambayo yanashuhudia umwagikaji wa damu kutokana na vita vya kikabila,” alisema Bw Kigame.

Hata hivyo, alitahadharisha uongozi wa Rais William Ruto dhidi ya kuendelea kulazimisha Wakenya kutozwa ushuru wa nyumba.

Bw Kigame alisema Wakenya wengi wamekabiliwa na ugumu wa maisha hivyo basi hakuna haja ya kulazimishwa kulipa ushuru wa nyumba wakati kama huu.

Kulingana na Kigame ni kwamba tatizo kubwa ambalo linawakabili Wakenya kwa sasa ni usalama wa chakula, ambapo wananchi wengi hawana chakula cha kulisha familia zao.

“Wakenya kwa sasa hawahitaji nyumba kupitia kwa huu mswada tata, kile wanataka ni chakula. Serikali inapaswa kuhakikisha usalama wa chakula badala ya kulazimisha watu kulipa ushuru wa nyumba kama ilivyo kwa mswada wa kifedha wa mwaka wa 2023,” alisema Bw Kigame.

Vile vile, kiongozi huyo alilezea hofu ya kutokea uhaba wa chakula nchini hata baada ya mavuno yanayotarajiwa mwishoni mwa mwaka.

Kwa muujibu wa Bw kigame ni kwamba gharama ya uzalishaji chakula inaendelea kupanda licha ya serikali kudai kuwapa wakulima mbolea ya bei nafuu.

“Hakuna vile tuanatarajia wakulima kupata mavuno bora ilhali gharama ya mafuta iko juu, pembejeo zingine za kilimo ziko juu huu ni unyang’anyi kwa wakulima wetu,” Bw Kigame ambaye pia ni mwanamuziki wa nyimbo za injili alisema.

  • Tags

You can share this post!

Sekta za elimu na miundomsingi zatengewa kiasi kikubwa cha...

Gachagua: Wakenya wengi wanaamini mikakati ya Rais...

T L