• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 7:55 PM
Ripoti ya upasuaji yabaini mwalimu aliyefariki siku chache baada ya kupata kazi alipondwapondwa kichwani

Ripoti ya upasuaji yabaini mwalimu aliyefariki siku chache baada ya kupata kazi alipondwapondwa kichwani

NA MWANGI MUIRURI

RIPOTI ya upasuaji wa mwili ya marehemu Andrew Njiru inaonyesha kwamba aliuawa kwa kupondapondwa kichwani, hii ikiashiria kwamba alishambuliwa.

Marehemu alikuwa mwalimu kitaaluma na alikuwa na umri wa miaka 35 alipokumbana na mauti yake katika Kaunti ya Murang’a.

Mzawa wa Kaunti ya Embu, mwalimu huyo alikuwa ameajiriwa rasmi na Tume ya Kuajiri Walimu nchini (TSC) katika usajili wa mwezi wa nane.

Alikuwa aanze kufundisha Septemba 1, 2023, katika shule ya Msingi ya Rutune iliyoko Murang’a lakini akapatikana ameuawa na kutupwa kwa mto siku mbili kabla ya kuingia rasmi darasani kuanza kutekeleza wajibu katika taaluma yake.

Mwili wake ulipatikana ukiwa umetupwa katika Mto Sagana katika kisa ambacho kiliashiria kuuawa.

Soma Pia: Mwalimu afariki siku chache kabla ya kuanza kazi aliyotafuta kwa muda

Ripoti ya daktari Kamatho Watenga aliyefanya operesheni hiyo inaonyesha kwamba “kichwa chake kilikuwa na majeraha mabaya na kilikuwa kimebondeka baada ya kupondwapondwa,”

Amesema pia mwalimu huyo alivuja damu kwa wingi hadi akafa.

Babake mwalimu huyo, Mzee William Mwangi sasa anaitaka idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) katika Kaunti ya Murang’a kuwajibikia haki ya mwendazake.

“Kwa sasa imebainika kwamba mtoto wangu aliuawa. Ninaomba sasa sheria ichukue mkondo wake. Kuna washukiwa ambao wamehusishwa na mauaji hayo na ambao kuna majirani wanaowajua. Ningetaka haki itendeke,” akasema.

Taarifa za mashahidi zinaonyesha kwamba Bw Njiru aliyekuwa amekodisha chumba cha malazi karibu na shule hiyo alichanganyikiwa wakati stima ilipotea nchini mnamo Agosti 27, 2023 na alipoenda dukani kununua mshumaa, akachanganyikiwa kurudi kwake na badala yake akaingia kwa majirani.

“Nimearifiwa kwamba alidhaniwa kuwa mwizi na ndugu wawili majirani wakamtandika hadi akafa na baadaye wakampakia ndani ya gari na wakatoweka naye,” akadai mzazi huyo.

Mkuu wa polisi wa Murang’a Mashariki Bi Mary Kasyoki alisema kwamba uchunguzi wa kubainisha kilichomuua Bw Njiru umeanzishwa.

  • Tags

You can share this post!

Omanyala atetemesha kwenye mbio za mita 100 katika...

Kenya yakaribia kujipatia Mtakatifu wake wa kwanza katika...

T L