RAIS William Ruto sasa anataka wabunge kuupigia kura Mswada wa Fedha 2023 hadharani utakapowasilishwa Bungeni wiki hii, huku akitishia kuwakabili wabunge watakaoupinga.
Akihutubu jana wakati wa hafla ya kurudisha shukrani kwa Waziri wa Mazingira, Soipan Tuya katika eneo la Leshuta, Narok Magharibi, Dkt Ruto alisema kuwa kura ya wazi itamsaidia kubaini wabunge wanaopinga ajenda yake ya maendeleo.
“Nilimsikia mbunge fulani akisema kuwa anataka kura hiyo kuwa ya wazi, ninaunga mkono wazo hilo. Nataka Wakenya wawajue viongozi ambao wanapinga juhudi zangu kuondoa ukosefu wa ajira. Wale watakaopinga mswada huo ni maadui wa maendeleo,” akasema Rais Ruto.
“Mimi nangoja kuona mbunge ambaye atapinga mpango tulio nao na atasimama upande gani wa hawa wananchi. Nawarai wabunge kuupitisha Mswada wa Fedha wa 2023 pamoja na Hazina ya Ujenzi kwani ni mzuri kwa Wakenya,” akaongeza Rais.
Akipigia debe Hazina ya Ujenzi, Rais alisema kuwa mpango huo utabuni ajira kwa mamilioni ya vijana nchini. Alisema kuwa utekelezaji wa Mpango wa Nyumba za Bei Nafuu ndiyo njia ya pekee ya kukabili ukosefu wa ajira nchini.
Akilalamikia hali ya ukosefu wa ajira, Rais Ruto alisema kuwa jumla ya vijana 5 milioni hawana ajira, huku idadi hiyo ikiongezeka kwa vijana 800,000 kila mwaka.
Elimu
“Huwa tunatumia Sh650 bilioni kila mwaka kuwapeleka watoto wetu shuleni lakini hawana ajira. Hivyo, lazima tuwe na mpango mahsusi kuhakikisha kuwa wanatumia ujuzi wao kuendeleza uchumi wa nchi,” akasema Dkt Ruto.
Kama sehemu ya Mswada wa Fedha 2023, kuna pendekezo ambalo limetolewa kuwa ikiwa mswada huo utatekelezwa, basi Wakenya watatozwa asilimia tatu ya mishahara yao ambapo fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wake.
Hata hivyo, pendekezo hilo limepingwa vikali, Wakenya wakilalamika kwamba tayari wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa ushuru.
Rais Ruto, hata hivyo, anashikilia kuwa Mswada huo utakuza sekta ya utengenezaji bidhaa. Amewataja wale wanaopinga mswada huo kama vile mrengo wa Azimio La Umoja kuwa wadanganyifu.
Alisema kuwa viongozi wa upinzani wanakubaliana na mswada huo lakini wanaupinga bila sababu maalum.
“Wakati wa kampeni za uchaguzi, kila mmoja wetu (Azimio na Kenya Kwanza) tulikuwa na mipango ya ujenzi katika manifesto zetu. Inanishangaza kuwa ikizingatiwa hawako serikalini, sasa wanaupinga mpango huo wa ajira,” akasema Rais.
Alisema kuwa mpango huo utahakikisha jumla ya Wakenya milioni saba wanaoishi katika mitaa ya mabanda wamepata makao.
Alisema kuwa miaka 60 iliyopita, Kenya ilikuwa katika nafasi sawa ya kiuchumi na mataifa mengine kama Singapore, Korea na Malaysia lakini kwa sasa raia wao wana nyumba nzuri ilhali Wakenya wana makazi duni.
Rais aliirai jamii ya Wamaasai kutouza ardhi yao ili kuishi maisha ya kifahari kwa wakati mfupi pekee.