• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Ruto apiga chenga Raila, Uhuru kuhusu mswada

Ruto apiga chenga Raila, Uhuru kuhusu mswada

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wandani wa Naibu Rais William Ruto jana walifaulu kuzuia kupitishwa kwa Mswada tata wa marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa baada ya kuwasilisha marekebisho mengi kwa mswada huo.

Wenzao wa mrengo wa handisheki walibaki hoi baada ya Naibu Spika, Moses Cheboi kusitisha mjadala kuhusu mswada huo ili kutoa nafasi ya kuchambuliwa kwa kina mapendekezo 10 kutoka kwa wabunge, wengi wao wakiwa wandani wa Dkt Ruto.

Wabunge waliopendekeza marekebisho kwa mswada huo ni; Aden Duale (Garissa Mjini), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Daniel Tuitoek (Mogotio), Owen Bay (Kilifi), Gitonga Murugara (Tharaka).Wengine ni; Silvanus Osoro (Mugirango Kusini), Caleb Kositany (Soy), Godfrey Osotsi (Mbunge Maalum, ANC) na mwenyekiti wa JLAC Muturi Kigano.

“Kwa sababu wabunge wamependekeza marekebisho mengi ambayo huenda yakachangia kuandikwa upya kwa mswada huu, naamuru maombi hayo yote yawasilishwe kwa kamati ya sheria (JLAC) ili yaoanishwe. Kwa hivyo, awamu ya tatu ya mjadala kuhusu mswada huu itafanyika katika kikao kijacho cha bunge hili,” Bw Cheboi akaeleza.

Lakini kiongozi wa wachache John Mbadi alipinga uamuzi huo akitaka wabunge warejelee mjadala kuhusu mswada huo saa kumi jioni lakini Bw Cheboi akakataa.“Mheshimiwa Spika uamuzi wako wa kuahirisha kikao hiki maalum unakiuka sheria za bunge hili.

Kikao hiki kiliitishwa kupitia ilani iliyochapishwa katika gazeti rasmi la serikali na haliwezi kusitishwa kabla ya shughuli iliyoratibiwa kutamatishwa,” akasema Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini. “Lakini Bw Mbadi hatuwezi kuendelea na shughuli hii kabla ya mapendekezo mengi ya marekebisho kushughulikiwa na kamati husika,” Bw Cheboi akajibu.

Hii ina maana kuwa mswada huo sasa utashughulikiwa tena mnamo Januari 25, wabunge watakaporejea kutoka likizo ya Krismasi na Mwaka Mpya.Hata hivyo, kiongozi wa wengi Amos Kimunya na Bw Mbadi wanaweza kumuomba Spika Justin Muturi kuitisha kikao kingine maalum kabla ya siku hiyo.

Awali, wabunge washirika wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walifaulu kufanikiwa kupitishwa kwa mswada huo katika awamu ya pili.Waliwalemea wabunge wa Tangatanga waliotaka kuzuia mswada huo kuvuka hatua hiyo muhimu.

Katika kura iliyopigwa kuamua suala hilo, wabunge wa handisheki walishinda kwa kura 113 dhidi ya kura 63 za wandani wa Dkt Ruto wanaoegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA).Hoja hiyo iliwasilishwa na Mbunge wa Limuru Peter Mwathi, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu usalama.

Awali, juhudi za Mbunge wa Tharaka Gitonga Murugara na mwenzake wa Dagorreti Kusini John Kiarie, kutaka mswada huo utupiliwe ziligonga mwamba.

You can share this post!

Karua apoteza raundi ya 2 katika kesi ya Waiguru

Eto’o asema ratiba ya AFCON haitabadilishwa

T L