• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Sababu ya mibuyu kuhusishwa na mashetani

Sababu ya mibuyu kuhusishwa na mashetani

NA KALUME KAZUNGU

MTI wa mbuyu hutambulika sana kwa sifa zake, hasa ukubwa wa mti huo na pia uwezo  wake wa kuishi  karne na karne.

Watafiti wanasema mbuyu unaweza kuishi kwa zaidi ya miaka 1,500.

Kukaa kwake mahali pia ni ishara tosha ya maisha kwa binadamu na wanyama.

Mbali na mti huo kuwa muhimu kwa mazingira yetu, ukubwa na kuishi kwake siku nyingi ni hali na vitu ambavyo vimechangia waja kuwa na fikra na dhana nyingi kuhusu, ikiwemo ile ya ushirikina.

Katika kijiji cha Midodoni eneobunge la Magarini katika Kaunti ya Kilifi ambapo mibuyu hupatikana kwa wingi, baadhi ya wazee waliohojiwa walisema si jambo geni kusikia waja wakilalamikia vituko vinavyoonekana mibuyuni, hasa nyakati za usiku.

Mibuyu kwa baadhi ya watu ni maficho ya mapepo na mashetani hii ikiwa dhana tu ambayo wakazi wa Lamu wanaizungumzia kwa undani. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw James Mwavula Mkoba, anasema tangu enzi za udogo wake amekuwa akisikia na mara nyingine hata kushuhudia viumbe wa ajabuajabu wakitoka ghafla mbuyuni wakati watu wanapotembea kwenye njia na vichochoro usiku, hasa maeneo ambapo mibuyu imesheheni.

“Twashukuru Mola kutujalia kuwa na mibuyu mingi eneo la kwetu. Twaichukulia Hali hii kuwa ni baraka kwetu. Si maeneo yote ya Kenya na ulimwengu utapata mibuyu mingi kama ilivyo hapa Midodoni. Cha kushangaza ni kwamba baadhi ya washirikina wamekuwa wakiitumia hii mibuyu visivyo. Utasikia eneo hili kuna mbuyu wa wachawi, mashetani, mapepo au mizimu. Waweza pitia mahali ukasikia sauti za ajabuajabu usiku. Mara nyingine hata unapata kondoo au ng’ombe akichomoka mbuyuni huku akiwaka moto. Hapo tayari utajua kwamba mbuyu huo ni wa mapepo au mizimu,” akasema Bw Mwavula.

Hata hivyo anasema ni kupitia watu kuzidisha imani kwa Mungu ambapo vituko hivyo vya mibuyu vimepungua eneo lao miaka ya hivi punde.

Bw Mwavula anasema kumekuwa na visa ambapo viongozi wa dini wamelazimika kukongamana na kuandaa maombi kwenye baadhi ya mibuyu kijijini Midodoni ili kutokomeza mapepo au mashetani kutoka kwenye miti hiyo.

“Miaka ya hivi punde tumejionea waja wakiifurahia mibuyu. Wengine hata hujenga nyumba zao chini ya mibuyu kwani matatizo yaliyokuwepo zamani ya mashetani au wachawi kuandama mibuyu yamefifia Na hata kutokomea kabisa. Watu wasiiogope mibuyu. Inatusaidia kuleta mvua Na kupamba madhari yetu si haba,” akasema Bw Mwavula.

Bw Samson Mwangi, mkazi wa Ndeu-Sabasaba, wadi ya Hindi, kaunti ya Lamu anakiri kuwepo kwa vituko mibuyuni, akitaja kuwa watu walioamini ushirikina kama vile uchawi na majini mara nyingi hutumia sana mibuyu kuzika au kuficha mazingaombwe yao.

Maeneo ya Ndeu na Sabasaba pia yamebahatika kuwa na mibuyu japo si mingi ikilinganishwa na Midodoni.

Bw Mwangi aidha anashikilia kuwa mbuyu hauna tatizo lolote ila mwenye tatizo hilo ni binadamu.

“Watu ndio wanaifanya hii mibuyu kuonekana kuwa miti ya kutisha. Sawasawa na unaposikia kuna paka jini Pwani,pia utapata mbuyu wa majini au mapepo. Hapa kiumbe kama paka hakina tatizo ila mtu ndiye hutumia kiumbe huyo vibaya, hivyo kumpaka tope au kisirani. Vivyo hivyo mbuyu hauna tatizo ila mja ndiye anayeutumia vibaya,hivyo kuupaka doa jeusi,” akasema Bw Mwangi.

Ikumbukwe kuwa tangu jadi mbuyu umehusishwa na stori nyingi sana za kufikirika. Kuna baadhi ya watu huamini kwamba kuna shughuli za kishirikina huendelea ndani ya mibuyu au labda ni sehemu wa washirikina kupumzika.

Utasikia hadithi za kutisha za zamani kwamba kwamba kuna mbuyu uliwahi kuwataka kimapenzi mabinti wa kijiji kiasi cha kwamba kila muda mabinti hao wakipita karibu, mbuyu huo ulidondosha matunda na kupuliza upepo mzuri na kuwapa kivuli lakini jitihada za mbuyu kuwavutia mabinti hao zikagonga mwamba.

Licha ya mbuyu kuonyesha upendo wote huo, mabinti hao walijiingiza kwenye mahusiano na wanaume wa kijiji na siku moja mabinti hao waliaga majumbani kwao kwenda kutembea na hawakurudi tena, ikisadikika mbuyu huo uliwafungia ndani ya shina lake milele kama kisasi.

Ni kupitia hadithi kama hizi ambapo pia zimechangia baadhi ya watu kuuogola mbuyu na hata kuepuka kabisa kuufikia punde wanapouona.

Pia ipo imani kwamba wanawake wanaoishi kwenye maeneo yenye mibuyu wana uwezo mkubwa wa kupata ujauzito kuliko wale wanaoishi maeneo yasiyo na mibuyu.

Pia ni tamaduni mpaka leo kwamba eneo lenye mti mkubwa kama mbuyu basi panafaa kuwa sehemu ya jamii au kijiji kukutana na kufanya mikutano ya hadhara.

Licha ya kuwepo kwa dhana na itikadi hizo, mbuyu bado utasalia kuwa mti wenye manufaa tele kwa waja.

Kwa mfano, tunda la mbuyu, lina rangi ang’avu ya mahameli ama ‘velvet’ na lina mbegu nyeusi ambazo zimezungukwa na unga mweupe ambao hutumika kutengeneza kinywaji safi kabisa cha ubuyu.

Unga huo pia unasaidia kuboresha afya ya ngozi, moyo na kusaidia kupungua kwa uzito mwilini.

Tunda la mbuyu pia lina virutubisho vingi kama madini ya chuma, kalshiamu na potashiamu ambavyo vina kiwango mara mbili zaidi ya vile vya kwenye mchicha.

Baadhi ya ripoti zinasema ule unga wa tunda la mbuyu una vitamini C mara 10 zaidi ya chungwa.

Aidha pia, mbegu za tunda la mbuyu ndiyo hutumika kutengeneza kiburudhisho cha kumung’unya kiitwacho ubuyu.

Isitoshe, majani ya mbuyu yamekuwa yakitumika kama mboga na baadhi ya jamii za barani Afrika.

Ni kutokana na hali hiyo ambapo mwaka huu wakazi na wanaharakati wa mazingira eneo la Pwani,hasa Kilifi,wamepinga kabisa pendekezo la mojawapo ya mashirika ya kimataifa ambalo lilitaka kununua mibuyu, kuikata na kuisafirisha ng’ambo kwa matumizi mbadala wakichacha kuwa maamuzi hayo hayafai kwani yataathiri mazingira.

  • Tags

You can share this post!

Maina Njenga ni mradi wa Gachagua kuzima umaarufu wa...

Wezi wa nguo wanaojifanya maafisa wa Kenya Power

T L