• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 3:23 PM
Sababu za Ruto kupinga vikali mswada wa vyama

Sababu za Ruto kupinga vikali mswada wa vyama

Na WANDERI KAMAU

Naibu Rais William Ruto na waandani wake wameapa kufanya kila wawezalo kulemaza juhudi za Kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuingia ikulu mwaka ujao.

Na mojawapo ya hatua hizo ni kuhujumu kupitishwa kwa Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ambao ungemwezesha Bw Odinga kuunda muungano mkubwa wa vyama vya kisiasa kwa urahisi.

Kulingana na wadadisi wa masuala ya kisiasa, hofu ya Dkt Ruto ni kwamba, ikiwa mswada huo utapitishwa jinsi ulivyo, basi utampa nguvu zaidi Bw Odinga, ikizingatiwa unapendekeza miungano ya kisiasa kugeuzwa kuwa vyama vya kisiasa.Bw Odinga anaongoza Mpango wa Azimio la Umoja, ambao amesema utageuzwa kuwa chama cha kisiasa–Azimio la Umoja Movement.

Bw Odinga alitoa kauli hiyo alipozindua rasmi azma yake ya urais Desemba 10 katika Uwanja wa Michezo wa Kasarani, jijini Nairobi. “Hofu ya kambi ya Dkt Ruto ni kwamba, ikiwa muungano huo utageuzwa kuwa chama cha kisiasa, basi utakuwa umemkweza kisiasa Bw Odinga na kumshusha Dkt Ruto kisiasa,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Tayari, vyama kadhaa vimeonyesha nia ya kujiunga na mpango wa Azimio la Umoja, miongoni mwao Jubilee, Kanu, PNU, DP kati ya vingine.Wadadisi wanasema ikiwa vyama hivyo vitajiunga na mpango huo, basi inamaanisha hilo litapanua uungwaji mkono wa Bw Odinga hata katika maeneo yanayoonekana kudhibitiwa kisiasa na Dkt Ruto.

Dkt Ruto amekuwa akifanya kampeni zake kupitia chama cha UDA, akishikilia lengo lake ni kukijenga kuwa chama cha kitaifa. Dkt Ruto amekuwa akisitiza kuwa, atabuni miungano na vyama vya kisiasa pindi baada ya uchaguzi wa 2022 kukamilika. Sababu nyingine inayomtia wasiwasi Dkt Ruto ni hofu ya urejeo wa Rais asiye na mamlaka au anayechukuliwa mateka na watu wachache.Wadadisi wanasema katika hali ambapo vyama kadhaa vitaungana na kubuni muungano wa kisiasa ambao baadaye utageuzwa kuwa chama cha kisiasa, itamlazimu Rais atakayechaguliwa kukidhi matakwa ya vyama vilivyoungana.

Wanafananisha hilo na miungano ya awali kama Narc, Cord, Nasa na Jubilee ambayo ilivunjika kutokana na mivutano ya vyama vya kisiasa.“Dkt Ruto analenga kuepuka matatizo na mivutano ya kisiasa ilivyoikumba miungano ya awali ya kisiasa, ambapo kila chama kilidai ‘mgao’ wake serikalini.

Hiyo ndiyo ilikuwa sababu kuu iliyochangia kuvunjika kwa miungano kama Cord, Nasa na Jubilee,” asema mdadisi wa siasa, Javas Bigambo.Anasema katika hali ambapo rais ndiye kiongozi wa chama kimoja, hilo litampa mamlaka na uwezo mkubwa wa kisiasa.

Akihutubu Jumatano katika Kaunti ya Garissa, Dkt Ruto aliekeza hofu yake kwamba ikiwa mswada huo utapitishwa ulivyo, basi utamfanya rais anayechaguliwa “kuzingatia matakwa ya watu wachache.” “Nawarai Wakenya kukataa njama za kuturejesha katika enzi ya rais atakayezingatia matakwa ya watu wachache,” akasema.

Ni kauli iliyoungwa mkono na mbunge Aden Duale (Garissa Mjini) ambaye ni miongoni mwa washirika wake wa karibu. Hata hivyo, wadadisi wanasema kinyume na kauli ya Dkt Ruto, lengo lake ni kuirejesha nchi katika enzi ya chama kimoja kama ilivyokuwa katika utawala wa Kanu.

Sababu ya tatu inayowasukuma washirika wa Dkt Ruto kuukataa mswada huo ni hofu kwamba, huenda wakafurushwa kutoka Chama cha Jubilee.Kulingana na sehemu 16 ya mswada huo, chama chochote cha kisiasa kiko huru kumfurusha kiongozi ama mwanachama yeyote anayeendeleza sera ama misimamo ya chama kingine.

Kulingana na wadadisi, hofu iliyokumba washirika wa Dkt Ruto ni kuwa, ikiwa mswada huo utapita, basi Jubilee itakuwa huru kuwafurusha ikizingatiwa wengi wao wamekuwa wakivumisha chama cha UDA.“Kisheria, mbunge anayefurushwa chamani huwa kwenye hatari ya kupoteza kiti chake, kwani Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) hutakikana kuandaa uchaguzi mdogo mpya katika eneobunge lake.

Hivyo, wandani wengi wa Dkt Ruto wanahofia kupoteza viti vyao ikiwa watafurushwa Jubiee kwa kujiunga na UDA,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.Sababu ya nne ni kuwa, Dkt Ruto analenga kulinda na kuendeleza maslahi yake kisiasa.

Wadadisi wanasema ikiwa mswada huo utapitishwa jinsi ulivyo, itamlazimu Dkt Ruto na waandani wake kuigeuza UDA kuwa muungano wa kisiasa, hivyo kuvuruga maslahi yao waliyowekeza kwenye chama. “Itamaanisha watavialika vyama vingine vya kisiasa. Hilo linamaanisha watagawana manufaa yoyote ambayo wangepata chamani —kama nafasi tofauti za uwakilishi, na ‘wageni,” asema Prof Macharia.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Serikali isirejeshe enzi za giza na kuua...

Sababu za Lamu kuibuka ‘ngome ya kijeshi’ Pwani

T L