• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
Sekta za elimu na miundomsingi zatengewa kiasi kikubwa cha mgao wa bajeti

Sekta za elimu na miundomsingi zatengewa kiasi kikubwa cha mgao wa bajeti

EDWIN MUTAI Na CHARLES WASONGA

SEKTA za elimu, miundomsingi na ulipaji deni ndizo zitafyonza sehemu kubwa ya mgao wa fedha katika Bajeti ya kwanza ya Rais William Ruto ya kima cha Sh3.6 trilioni, Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti (BAC) imefichua.

Kamati hiyo, kwenye ufichuzi usio wa kawaida, inasema kuwa imetenga Sh600 bilioni kwa sekta ya elimu, Sh400 bilioni kwa sekta ya miundomsingi, kawi na habari, na Sh628.3 bilioni zimetengwa ili kulipia madeni ya umma; yaliyokopwa humu nchini na katika nchi za kigeni.

“Takwimu ambazo tunatoa ndizo halisi na hata zikibadilika basi kutakuwa na mabadiliko madogo tu. Tumeandaa bajeti ya kitaifa ya kima cha Sh3.599 trilioni. Tunatarajia kukusanya mapato ya Sh2.57 trilioni, tunatarajia kupokea Sh322 bilioni kama mikopo na Sh42 bilioni kama ruzuku kutoka kwa wafadhili,” mwenyekiti wa BAC Ndindi Nyoro akasema.

Bw Nyoro, ambaye ni Mbunge wa Kiharu alitoa maelezo hayo Jumatano kwenye kikao na wanahabari katika Majengo ya Bunge, Nairobi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti (BAC) Ndindi Nyoro. PICHA | MAKTABA

Alisema kati ya bajeti hiyo ya mwaka wa kifedha wa 2023/2024, Sh2.16 trilioni zimetengewa Serikali Kuu, Sh40.4 bilioni zimetengewa Bunge na Sh22.9 bilioni zimetengewa Idara ya Mahakama.

Hazina ya Huduma za Pamoja (CFS) – inayotumika kulipa riba kwenye mikopo, pensheni na tume za kikatiba – imetengewa Sh986.2 bilioni huku serikali za kaunti zikitengewa jumla ya Sh385.4 bilioni kama mgao wa usawa na Sh44.2 bilioni kama mgao wa kufadhili miradi mahususi (conditional allocations).

Kamati hiyo ya BAC, ambayo itawasilisha ripoti yake ya mwisho Jumanne, Juni 6, 2023, Bunge litakaporejelea vikao vyake kabla ya kusomwa kwa bajeti, Juni 15, ilisema kuwa bajeti hii ina upungufu wa Sh680 bilioni. Upungufu huo hufahamika kama nakisi kwenye makadirio ya bajeti.

Pengo hilo litajazwa kupitia ukopaji kutoka mashirika ya kifedha ya humu nchini na mataifa ya ng’ambo.

“Tumetenga Sh1.5 trilioni za matumizi ya kawaida katika serikali ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na matawi ya serikali kuu, Bunge na Idara ya Mahakama,” akasema Bw Nyoro.

Aliongeza kuwa Sh728 bilioni zimetengwa kufadhili miradi ya maendeleo katika mwaka ujao wa kifedha ambao unaanza Julai 1, 2023.

Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u aliambia kamati ya BAC kwamba mgao wa hazina ya CFS zinajumuisha Sh628.3 bilioni kulipa riba ya mikopo ya humu nchini, Sh146. 9 bilioni za kulipa riba ya mikopo ya kigeni na Sh210 bilioni za kulipa pensheni, mishahara na marupurupu.

Profesa Ndung’u alisema matumizi ya kawaida ya Sh2.477 trilioni ni asilimia 15.5 ya jumla ya utajiri wa kitaifa (GDP) ilhali mgao wa fedha za maendeleo ni Sh689.1 bilioni, sawa na asilimia 4.2 ya Jumla ya Utajiri wa Kitaifa (GDP).

“Mgao kwa serikali za kaunti unakadiriwa kuwa Sh429.7 bilioni (asilimia 2.6 ya GDP) huku mgao kwa Hazina ya Dharura ikikadiriwa kuwa Sh2.8 bilioni,” Profesa Ndung’u akasema.

Alieleza kuwa kutokana na kujitolea kwa serikali kupunguza matumizi na mikakati ta kuongeza viwango vya ukusanyaji wa mapato iliyowekwa, upungufu kwenye bajeti, ukijumuisha ruzuku, inakadiriwa kuwa Sh663.5 bilioni au asilimia 4.1 ya GDP katika mwaka wa kifedha wa 2023/24.

“Pengo kwenye bajeti katika mwaka wa kifedha wa 2023/24 litajazwa na ukopeshaji wa Sh131.5 bilioni (au asilimia 0.8 ya GDP),” Profesa Njuguna akasema.

Bw Nyoro alifichua kuwa sekta ya Elimu imetengewa Sh604 bilioni kwa sababu ya ongezeko la mgao kwa Shule ikizingatiwa kuna Sekondari za Msingi (JSS).

“Mgao wa juu zaidi ni kwa sekta ya elimu, itakayotengewa asilimia 27 ya bajeti ya kitaifa. Tumetenga fedha kufadhili mafunzo ya kiufundi na kuajiri wakufunzi na vyuo vikuu pia vitapokea mgao zaidi wa fedha katika bajeti hii,” Bw Nyoro akasema.

Alisema sekta za miundomsingi, barabara, kawi na ICT zitapokea mgao wa pili kwa ukubwa wa Sh400 bilioni.

“Tumetenga pesa zaidi kwa sekta ya barabara kwa sababu wanakandarasi wametia saini kandarasi za thamani ya zaidi ya Sh900 bilioni. Tumepunguza thamani ya kandarasi hizi hadi Sh600 bilioni. Tumesimamisha utekelezaji wa miradi mipya ya barabara na pesa tulizotenga kwa sekta ya barabara zitatumika kukamilisha miradi ambayo tayari imeanza,” Bw Nyoro akasema.

“Hatutaki kuwe na miradi ya barabara iliyokwama. Tunataka kukamilisha miradi yote inayoendelea,” Mbunge huyo wa Kiharu akasisitiza.

Wakati huo huo, Bw Nyoro alisema kuwa kamati yake (BAC) imetenga pesa zaidi kwa miradi 10 ya kuongeza thamani ikiwemo ile inayopatikana katika sekta ya kilimo.

“Aidha, Sh4.5 bilioni zimetengwa kwa mpango wa utoaji mbolea kwa bei nafuu na mpango wa kilimo kidijitali,” akaeleza.

Bw Nyoro alisema kamati yake inafuatilia kwa makini deni la kitaifa kuhakikisha kuwa serikali haikopi kupita kiasi.

“Wakati huu tunafuatilia deni la kitaifa la Sh10 trilioni, ambalo ni la juu zaidi. Kuna pendekezo la kuweka kiwango cha ukopaji kuwa kima cha asilimia 55 ya Jumla ya Utajiri wa Kitaifa (GDP) ambacho ni Sh16 trilioni. Hili ni suala ambalo litashughulikiwa na Bunge,” Bw Nyoro akasema.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto awasili akiwa amechelewa Embu kuadhimisha...

Reuben Kigame aitaka Azimio isitishe vitisho kugawa nchi

T L