• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Serikali ya wakaidi wa sheria

Serikali ya wakaidi wa sheria

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI imeonywa kuwa mazoea ya maafisa wake, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta ya kukaidi maagizo ya mahakama na utawala wa sheria ni hatari kwa usalama wa kitaifa.

Kulingana na watetezi wa sheria, mazoea hayo yanaweza kuchochea vurugu nchini iwapo raia watawaiga wakuu serikalini katika kupuuza mahakama sheria.

Kulingana na Jaji Mkuu (Mstaafu) Dkt Willy Mutunga, ukaidi wa sheria miongoni mwa maafisa wa serikali na wengine wenye ushawishi ni jambo la kutia wasiwasi, kwani linaweka msingi wa taifa lisiloweza kuthibitiwa kisheria.

Dkt Mutunga amesema hayo kufuatia hatua ya majuzi ya serikali kupuuza agizo la korti lililotaka wakili Miguna Miguna, anayeishi Canada kuruhusiwa kurejea nchini.

Dkt Miguna alipaswa kuwasili Kenya mnamo Jumanne asubuhi katika jaribio lake la tatu kufanya hivyo, lakini akazimwa baada ya kampuni ya ndege ya Ufaransa kupata ilani ya kutombeba kutoka kwa serikali ya Kenya.

Msomi wa sheria, Dkt Sylvia Kangara anasema kuwa Katiba inapasa kuheshimiwa na kila raia wakati wote bila kujali tabaka lake, wala sio tu wakati inapompendelea.

“Katiba haiwezi kuitwa Katiba iwapo inalinda tu wale wanaokubaliana na maoni yako ama marafiki. Haiwezi kuitwa Katiba iwapo unaitumia kama swichi ya kuwasha na kuzima stima,” akasema Dkt Kangara.

Haki za raia

Kulingana na Dkt Mutunga, kati ya mihimili mitatu ya serikali, ni mahakama pekee inayotetea haki za raia dhidi ya dhuluma za maafisa wa serikali: “Serikali Kuu na Bunge hazijali maslahi ya raia, mwokozi wetu kwa wakati huu ni mahakama,” alisema.

Wakili Nelson Havi naye alisema Wakenya wanafaa kuwa na hofu na kukasirishwa na hatua ya serikali ya kupuuza sheria: “Wanasiasa wamekuwa wakifanya mikutano ya kampeni na kutoa ahadi za kila aina lakini hakuna anayeahidi kuheshimu haki za raia na kulinda Katiba. Hii inafaa kutupatia wasiwasi.”

Kisa cha serikali kukaidi mahakama kuhusu Bw Miguna ni kimoja tu kati ya misururu ya maagizo ambayo serikali imekuwa ikidharau.

Rais Kenyatta amekuwa akilaumiwa zaidi kwa mtindo wa kukaidi maamuzi ya mahakama.

Kati ya maagizo aliyopuuza ni kuharamishwa kwa Idara ya Huduma ya Jiji la Nairobi (NMS) na uteuzi wa wakuu wa mashirika ya serikali ambao alifanya kuanzia 2018.

Kabla ya uamuzi huo, mahakama iliamua kwamba nyadhifa za mawaziri wasaidizi ambazo Rais Kenyatta alibuni ni haramu kwa kuwa hazitambuliwi katika Katiba, lakini badala ya kutii aliendelea kuteua mawaziri wasaidizi zaidi.

Rais Kenyatta amekataa kuapisha majaji sita walioteuliwa na JSC mnamo 2019.

Ilimchukua kiongozi wa nchi miaka miwili kukubali kuapisha majaji wengine 36 licha ya mahakama kuamua mara mbili kwamba alikuwa amekiuka katiba kwa kukataa kuwaapisha.

Polisi wakaidi Mutyambai

Rais pia amepuuza uamuzi wa mahakama kuwa kukabidhi usimamizi wa kiwanda cha nyama cha Kenya KMC kwa jeshi hakukuwa halali.

Serikali pia imepuuza maagizo mengine kama vile kulipa walimu waliostaafu mnamo 2007 marupurupu yao pamoja na kufidia waathiriwa wa dhuluma za serikali.

Maafisa wa polisi pia ni miongoni mwa watumishi wa umma wanaokaidi hata mkubwa wao.

Mnamo Septemba 19, 2021, Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai aliagiza polisi kuondoa vizuizi vya barabarani, lakini hadi sasa wanaendelea kuviweka na kuvitumia kudai hongo kutoka kwa madereva.

Wafanyikazi wa serikali pia wamekuwa wakikaidi sheria watakavyo hasa barabarani ambako wanavunja kanuni za trafiki kiholela

You can share this post!

MKU yaendesha kongamano la kibiashara

Pigo kwa ‘mpango wa kando’ Uhuru akisaini...

T L