• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
Serikali yagundua ruzuku kwa mafuta inafaa

Serikali yagundua ruzuku kwa mafuta inafaa

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI mnamo Agosti 14, 2023, ilidumisha bei za bidhaa za petroli ambazo zimetumika tangu Julai 14, 2023, baada ya kurejesha mpango wa kutoa ruzuku kwa bei za bidhaa hizo.

“Kwa hivyo, kuanzia Jumanne Agosti 15, 2023, bei za mafuta aina ya petroli, dizeli na mafuta taa hazitabadilia. Bei hizo zitasalia Sh194.68 kwa lita moja ya petroli, Sh179.67 kwa lita ya dizeli na Sh169.48 kwa lita ya mafuta taa jijini Nairobi kuanzia siku hiyo,” Mamlaka ya Kudhibiti Bei za Kawi na Bidhaa za Petroli (EPRA) ikasema kwenye taarifa iliyotumwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Daniel Kiptoo.

Serikali ya Rais William Ruto ilikuwa imetupilia mbali mpango wa kutoa ruzuku kwa bei za mafuta kuanzia Mei 2023, hatua iliyochangia bei za bidhaa za petroli kupanda kwa hadi Sh13 kwa lita moja.

Kulingana na EPRA, kurejeshwa kwa ruzuku kwa bei za mafuta kunalenga kuwakinga Wakenya kutokana na makali ya kupanda kwa bei kulikochangiwa na kupanda kwa bei za bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa.

“Ili kuwakinga wateja kutokana na bei za juu za mafuta zilizochangiwa na kuongezeka kwa bei ya mafuta yanayoagizwa kutoka nje, serikali imeamua kutoa ruzuku kwa bei za mafuta katika kipindi cha Agosti-Septemba,” taarifa ya EPRA ikasema.

Hii ina maana kuwa chini ya mpango huu mpya, serikali itaziruzuku Kampuni za Kuuza Mafuta (OMCs) kwa kuweka mkakati wa kutoongeza bei za bidhaa za mafuta.

Ikiwa serikali haingetoa ruzuku, inadiriwa kuwa bei za petroli, dizeli na mafuta taa zingeongezeka kwa Sh7.33, Sh3.59 na Sh5.74, kwa lita moja mtawalia.

Hii ina maana kuwa bei ya lita moja ya petroli jijini Nairobi ingepanda kutoka Sh194.68 hadi Sh202.01.

Nayo bei ya dezeli ingapanda kutoka 179.67 kwa lita hadi 183.26 huku bei ya mafuta taa ikiongezeka kutoka Sh169.48 hadi Sh175.22.

Ongezeko hilo lingeibua malalamishi makubwa kutoka kwa raia kwa sababu lingechochea kupanda kwa gharama ya maisha hata zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Caroli Omondi: “Komeni kunitusi kwa jina la marehemu...

Polisi wasaka mshukiwa anayetembea akiwa amejihami kwa shoka

T L