• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:54 PM
Serikali yakubali tope la Shakahola

Serikali yakubali tope la Shakahola

MARY WAMBUI Na ALEX KALAMA

SERIKALI imekubali kubeba lawama kwa kushindwa kuzuia kutokea kwa vifo vya watu kwenye msitu wa Shakahola.

Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki akihutubia wanahabari jijini Nairobi leo Jumatano amesema kulikuwa na utepetevu na maafisa wa usalama walizembea wakashindwa ‘kugundua’ na kuzuia maafa ya wanaoaminika kuwa walikuwa wafuasi wa mhubiri Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International.

Inadaiwa mhubiri huyo alikuwa akiwashawishi wafuasi wake wafunge hadi wafe ili wakutane na Yesu. Yuko kizuizini.

Hadi kufikia jana Jumanne, mshirikishi wa Pwani Rhoda Onyancha alisema idadi ya watu waliofariki kwa kufuata mahubiri ya kupotosha ilikuwa imefika 243 baada ya mtu mmoja zaidi kufariki mnamo Jumatatu wiki hii.

“Tumewaokoa wanaume wawili hii leo Jumanne wakiwa wamedhofika kiafya na tumewakimbiza katika hospitali ya Malindi ili kupata matibabu. Kufikia sasa waliokolewa ni 95 lakini wale ambao wako hai ni 94 kwa sababu mmoja aliaga,” akasema Bi Onyancha.

Afisa huyo wa utawala alisema kuwa idadi ya familia zinazotafuta jamaa zao waliopotea bado imesalia ile ya 613 huku idadi ya watu waliochukuliwa vipimo vya DNA ikiwa ni 93.

Mbali na hayo Bi Onyancha alidokeza kuwa operesheni ya kuwasaka manusura waliosalia ndani ya msitu huo bado inaendelea na inafanyika usiku na mchana.

Jumla ya miili 36 ilifanyiwa upasuaji mnamo Jumanne ambapo ilibainika watu wawili walifariki aghalabu kwa kuuawa. Mmoja alinyongwa na mwingine alifariki kwa kupigwa nyuma ya kichwa.

Hata hivyo imebainika kuwa 15 kati yao walifariki kutokana na ukosefu wa chakula na maji nao wengine 18 haikuweza kutambulika chanzo cha vifo vyao kutokana na hali halisi kwamba miili ilikuwa imeoza sana.

Akizungumza na wanahabari mnamo Jumanne katika mochari ya Hospitali Kuu ya Malindi, mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor alieleza kuwa, mwili mmoja uliofanyiwa uchunguzi ni wa mtu mmoja ambaye aliokolewa Jumatatu ila akafariki kutokana na ukosefu wa maji na chakula kando na kupatikana kuwa alikua anaugua kifua kikuu.

“Tumefanya upasuaji wa jumla ya miili 36 ambapo miili 10 kati ya 36 ilikuwa ya watoto na mwili mmoja ulikuwa wa mtu aliyeaga dunia wakati akipokea matibabu katika hospitali ya Malindi baada ya kuokolewa Jumatatu,” alisema Bw Oduor.

Wakati huo huo Dkt Johansen ameeleza kuwa kati ya miili 10 ya watoto iliyofanyiwa uchunguzi imebainika kuwa mmoja ulikuwa ni wa kijusi na mwingine wa mtoto wa umri wa chini ya mwaka mmoja.

Awamu ya pili ya upasuaji wa maiti imekamilika leo Jumatano.

Kwenye msitu wa Shakahola mnamo Jumanne watu wawili waliokolewa wakiwa katika hali mbaya na kukimbizwa hospitalini ili kupata matibabu ya dharura.

  • Tags

You can share this post!

Waliovamia shamba la familia ya Uhuru Kenyatta kukamatwa

Azimio wazima mazungumzo ya maridhiano hadi wakati...

T L