• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Serikali yaonya walimu wanaosisitiza sare zinunuliwe shuleni au kutoka kwa maduka fulani

Serikali yaonya walimu wanaosisitiza sare zinunuliwe shuleni au kutoka kwa maduka fulani

NA CHARLES WASONGA

WALIMU wakuu ambao watawalazimisha wazazi kununua sare kutoka kwa maduka fulani au ndani ya shule zao sasa wataadhibiwa vikali.

Hii ni baada ya Wizara ya Elimu kupiga marufuku mwenendo huo ambao ni ukora wa kuwapunja wazazi kwa kuuziwa sare na vifaa vingine hitajika kwa bei ghali kuliko bei ya kawaida. Wazazi huwanunulia watoto wao bidhaa hizo.

Kwenye taarifa iliyotolewa Mei 30, 2023 Katibu katika Wizara ya Elimu Belio Kipsang anasema kuwa mwenendo huo, ambao wazazi wametoa malalamiko kuuhusu, ni kinyume cha Sheria ya Elimu ya Kimsingi na kanuni kuhusu Elimu ya Msingi 2015.

Nakala za barua hiyo zilitumwa kwa walimu wakuu, wakurugenzi wa elimu katika ngazi za kaunti na kaunti ndogo na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC).

“Wizara itafuatilia suala hili na kuandaa majina ya shule ambazo hazitatimiza agizo hili ili zichukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” Dkt Kipsang’ akasema.

Katibu huyo wa Wizara ya Elimu anayesimamia Idara ya Elimu ya Msingi, alisema kuwa wazazi wako huru kununua sare na mahitaji mengine ya wanafunzi kutoka kwa maduka wanayotaka.

Dkt Kipsang’ aliweka wazi kwamba kulingana na Sheria ya Elimu ya Msingi, malengo ya elimu bila malipo na kanuni nambari 67 (3) ya Kanuni kuhusu Elimu ya Msingi, 2015, hakuna shule ambayo inaruhusiwa kuamua mfanyabiashara au duka ambalo wazazi au walezi wanafaa kuenda kununua sare na vifaa vingine vya shule.

Wazazi wamekuwa wakiwashutumu walimu wakuu kwa kuwalazimisha kununulia watoto sare na vifaa vya shule kutoka kwa maduka fulani kwa bei ya juu.

Wazazi hao pia wanadai kuwa wasimamizi wa shule wana uhusiano fulani na maduka hayo na wao hufaidi kutokana na bei hizo za juu.

Baadhi ya walimu wakuu pia hulazimisha wazazi kununua mahitaji hayo katika shule zao, hali ambayo huashiria kuwa shule hizo hushirikiana na watengenezaji au wawasilishaji wa bidhaa hizo.

Hii ndio maana katika baadhi ya shule, wazazi hulazimishwa kununua long’i kwa bei ya Sh870 kila moja. Hii ni licha ya kwamba vazi hilo linaweza kugharimu Sh350 katika soko la wazi.

Vile vile, baadhi ya wazazi hulazimishwa kununua shati moja kwa Sh530 ilhali shati hilo linaweza kuuzwa kwa Sh250 kila moja katika maduka mengine.

Aidha, duru zinasema kuwa katika baadhi ya shule za upili, sweta inauzwa kwa Sh1,500 ilhali vazi hilo linaweza kuuzwa kwa bei ya chini ya Sh800 katika maduka mengine.

  • Tags

You can share this post!

Watu 288 wafariki baada ya treni tatu kugongana nchini India

Msikiti wa Jamia waandaa siku ya hamasisho, Wakristo...

T L