• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:30 AM
Shakahola: Kindiki afungua rasmi awamu ya pili ya upasuaji wa maiti

Shakahola: Kindiki afungua rasmi awamu ya pili ya upasuaji wa maiti

NA FARHIYA HUSSEIN

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki mnamo Alhamisi amefungua rasmi awamu ya pili ya shughuli ya upasuaji wa maiti zilizofukuliwa kutoka kwa msitu wa Shakahola.

Prof Kindiki amesema shughuli ya upasuaji inafanyika katika mochari ya Hospitali Kuu ya Malindi na inaongozwa na mwanapatholojia mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor ambaye atakuwa akitoa taarifa saa kumi na moja jioni.

Jumla ya miili 129 itafanyiwa upasuaji kubaini kilichosababisha vifo vya watu hao wanaoaminika walikuwa wafuasi wa mahubiri ya Pasta Paul Mackenzi wa kanisa la Good News International. Kwenye awamu ya kwanza ni miili 112 iliyofanyiwa upasuaji.

Hii inamaanisha kufikia Alhamisi idadi ya watu waliothibitishwa kufariki ni 241.

Ingawa hivyo, waziri Kindiki amesema kikosi cha uokozi kilipata mifupa mikavu ya watu watano iliyopatikana baada ya kusitishwa kwa ufukuaji zaidi wa makaburi ndani ya chaka hilo.

“Jana Jumatano, mtu mmoja aliyekuwa ameokolewa kwenye msitu wa Shakahola alifariki akiwa hospitalini kwa sababu alikataa kula chakula,” amesema waziri.

Kufikia sasa watu waliookolewa ni 91. Maafisa na wataalam wamekusanya sampuli za vinasaba vya DNA kutoka kwa familia 93. Familia 19 zimeunganishwa na wapendwa wao. Jumla ya watu 34 wamekamatwa kufikia sasa.

Shughuli ya ufukuaji itarejelewa baada ya kukamilika kwa awamu ya pili ya upasuaji.

Na wakati huo huo, waziri amesema kuna thibitisho kuonyesha kwamba kuna makaburi zaidi ndani ya msitu wa Shakahola.

Amefichua kwamba baadhi ya wafuasi wa imani potovu ambao wangali hai wanajaribu kukwepa kwenye shamba hilo linalodaiwa kuwa la mhubiri Paul Mackenzie na kwamba serikali imefanikiwa kuokoa baadhi.

Lakini wengine wamefika maeneo ya Galana Kulalu na katika mbuga ya wanyama ya Tsavo Mashariki.

“Tutatumia teknolojia za kisasa kuhakikisha tunafanya msako katika msitu wote na maeneo ya karibu,” amehakikisha waziri akisema kuwa watu wengine zaidi wamekamatwa na itachukua muda kubaini nini hasa kilitokea na vitengo vipi vya usalama na utawala vilizembea.

Ameahidi kwamba ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma itafanya kila iwezalo kuhakikisha waliotekeleza unyama huo wanafunguliwa mashtaka.

  • Tags

You can share this post!

Shakahola: Awamu ya pili ya upasuaji maiti yaanza leo...

Serikali yatwaa Sh102 milioni alizopokea mwanadada kutoka...

T L