• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Silvanus Osoro alaumu serikali ya Kenyatta kwa masaibu ya Margaret Nyakang’o

Silvanus Osoro alaumu serikali ya Kenyatta kwa masaibu ya Margaret Nyakang’o

NA MARY WANGARI

KUNDI la wabunge kutoka Kisii limemtetea vikali Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakang’o, likidai kuwepo maafisa nje na ndani ya serikali wenye nia ya kuhujumu utawala wa Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Wakiongozwa na Kiranja Mkuu katika Bunge la Kitaifa, Silvanus Osoro, waundasheria hao wametaja hatua ya kumkamata hadharani Bi Nyakang’o kama njama za kisiasa wakiapa kumtetea kisheria.

Waundasheria hao wamedai wahusika, wanaojumuisha maafisa wa serikali iliyopita waliosalia mamlakani, wamekuwa wakitumia nyakati ambapo Rais Ruto amesafiri nje ya nchi na Naibu wake ameshughulishwa na masuala ya El Nino, kuwalenga maafisa wakuu wa umma kwa nia ya kusawiri vibaya utawala wa UDA.

“Tumegundua katika siku za hivi karibuni kama miezi sita iliyopita na baada ya kufuatilia kwa makini tukio hili kwamba kuna makundi ndani na nje ya serikali wanaotumika kula njama za kuhujumu nia njema ya Rais na Naibu Rais ya kusawazisha wanajamii kwenye ajira katika asasi za umma,” alisema Bw Osoro.

Mbunge huyo wa Mugirango Kusini alisema kuwa Kiongozi wa Taifa na Naibu wake hawana habari kabisa kuhusiana na masaibu yaliyomkumba Mdhibiti wa Bajeti kwa kuwa “Rais alikuwa amesafiri naye Naibu Rais alikuwa anashughulikia El Nino ambayo tunavyojua imesababisha majanga.”

“Leo Rais atawasili na sisi kama viongozi tutamwona kwa sababu tunajua hajui, tulipata habari pia naibu rais hajui, EACC pia hawajui.”

Mbunge huyo alirejelea kisa cha hivi majuzi ambapo Mkurugenzi wa Ukumbi wa Kitaifa wa Bomas, Peter Gitaa ikiwemo maafisa wengine 11 walisimamishwa kazi kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Walikashifu namna ambavyo EACC ilimkamata Bi Nyakango alipokuwa katika ziara ya kikazi Mombasa wakisema ni kinyume na msimamo wa serikali ya Kenya Kwanza kuhusu kulinda hadhi ya maafisa wa umma.

“Ziara hiyo ililipiwa na walipa ushuru, mbona hawangesubiri hadi arejee Nairobi au wamchukue nyumbani kwake, aina hii ya kufedhehesha sio tulichoahidi watu wetu, nadhani hata si jambo ambalo Rais na Naibu Rais wanataka. Haya ni mambo tuliyopinga tulipokuwa tukifanya kampeni kama muungano wa Kenya Kwanza. Tulisema hakutakuwa tena na kuandamwa kisiasa, watu hasa maafisa wakuu wa umma hawataaibishwa hivyo,” alisema.

“Haingekuwa vigumu kumwagiza Bi Nyakango kujiwasilisha kwa EACC au popote pale kwa sababu ni mtumishi wa umma na kisha kumfikisha kortini. Lakini mnasubiri, mnamkamata kama mwizi, mtu ambaye amehudumia taifa hili, hatuwezi kukaa kimya. Tulimpiga msasa alipoteuliwa na akaidhinishwa kuhudumu katika wadhifa wake, kwa nini masuala hayo hayakujitokeza wakati huo?”

Waundasheria hao sasa wameapa kusimama imara na Bi Nyakango wakiwalaumu baadhi ya watu wenye dhana kwamba baadhi ya wanajamii hawafai kushikilia nyadhifa muhimu serikalini.

 

  • Tags

You can share this post!

LSK yawinda mawakili 21 bandia

Mshukiwa wa ulghai alivyotiririkwa na machozi akililia...

T L