• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Simulizi ya bodaboda aliyeponea kifo mwenzake akifariki kwenye beti ya Sh200 pekee

Simulizi ya bodaboda aliyeponea kifo mwenzake akifariki kwenye beti ya Sh200 pekee

NA MWANGI MUIRURI

MNAMO Agosti 23, 2023, ilikuwa siku ambayo Bw Erastus Kamau wa umri wa miaka 23 aliponea kifo katika kisa anachokitaja kama cha upumbavu mkuu wa kushiriki mashindano ya bodaboda.

“Mwenzangu ambaye tulikuwa katika sekta ya bodaboda pamoja alinipata katika steji ya Murang’a na akanichongoa kwamba sikuwa nimeafilia viwango vya udereva wa nduthii na pia niliyokuwa nikiendesha ilikuwa mzee sana kiasi cha kuweza tu mwendo wa konokono,” asema.

Kusikia hivyo, Bw Kamau pia wa miaka 23 alimwambia mwenzake huyo kwa jina Edwin Kibata kwamba alikuwa amenoa sana katika ukadiriaji wake na ikiwa alikuwa anajielewa, aweke beti ya Sh200 washindane.

“Alikubali. Masharti yalikuwa atakayefika wa kwanza katika steji ya Kabuta iliyoko takribani kilomita tatu kutoka mji wa Murang’a ukielekea Sagana ndiye angepokea hizo pesa,” asema.

Mashindano hayo yaliishia Bw Kibata kuaga dunia wakiwa wamebakisha mita kama 50 wafike kwa steji ya Kabita.

“Mbio zikuwa za kukata na shoka. Tulikimbizana huku sote wawili tukiwa tumeinama ili kuhepa upepo mkali. Mimi niliangalia spidomita yangu na nikaona nilikuwa katika mwendo wa kilomita 140 kwa saa moja. Ni gurudumu la mbele la pikipiki yangu ambalo lilikuwa mbele ya mpinzani wangu,” asema.

Bw Kamau anasema kwamba “nilikuwa nashindana naye papa kwa hapa na ni gurudumu tu lilikuwa mbele. Ili kushinda, ni lazima dereva na pikipiki yake wangefika kwa steji hiyo ya Kabuta wakiongoza”.

Katika harakati za kusaka mbinu ya mwisho ya kuweza kufika akiwa mshindi, Bw Kamau anasema kwamba mbele yao kulikuwa na lori la kubeba mizigo.

“Mimi nilijua tu ushindani ungetwaliwa katika mbinu ya kupita lori hilo. Ni kama sote tulifanya hiyo hesabu kwa kuwa nilipoingia upande wa kulia ili nipite lori hilo, naye mwenzangu aliingia tu upande huo wa kulipita,” asema.

Bw Kamau anaongeza kuwa wote wakiwa upande wa kulia,  yeye ndiye alikuwa upande wa mwisho wa lami huku naye Bw Kibata akiwa kando yake kushoto.

“Hesabu yangu ilikuwa nikienda kupita lori hilo, nisonge upande wa kushoto ili nimnyime mpinzani wangu nafasi ya kulipita na katika hali ya kunipisha kwanza nipite, nimalize wa kwanza mita hizo 50 zilizosalia,” asema.

Lakini  shetani aliingia ndani ya hiyo hesabu na kuivuruga kwa mpigo mmoja.

“Nilikuwa niko karibu kufikia lori hilo na nianze kulipita huku nikilisongea ili nifunge mwanya wa mwenzangu kulipita mbele yangu kwa kuwa bado gurudumu langu la mbele lilikuwa limetangulia… Ghafla, lori hilo likaanza kuingia kwa barabara unganishi iliyokuwa upande huo wa kulia,” asema.

Eneo la Kabuta ambapo ajali iliyomuua Bw Edwin Kibata na ikamjeruhi Bw Erastus Kamau ilitokea Agosti 23, 2023. Waligonga lori lililokuwa likiingia katika barabara hii unganishi iliyo kulia. PICHA | MWANGI MUIRURI

Mashindano yakageuka kuwa dharura ya kujiokoa.

“Mimi niliona gurudumu la lori hilo la mbele kulia limetoka kwa barabara ya lami… Nami nikatoka kwa lami spidi yangu ikiwa ya juu… Nakumbuka tu nikisikia mlio wa gurudumu la pikipiki yangu likigonga bampa ya lori hilo. La kusikitisha ni kwamba nilimsikia mwenzangu Kibata akipiga nduru na hayo menginme sikuyajua,” asema.

Bw Kamau anasema kwamba alijisikia akiwa angani pikipiki akiiacha ardhini, lakini huko kupaa kukafifia na akaanza kurejea chini.

“Sijui huku kupaa na kushuka kuliisha namna gani kwa kuwa niliona giza limegubika uhai wangu, nikaona kama nimeona malaika wakiwa wamevalia mavazi meupe huku upande mwingine kukiwa na moto mkubwa na kabla niamue pa kuelekea, hali ikiwa dhahiri kwamba kwa moto ni kule tunasikia kwa Shetani na kwa waliovalia meupe kukiwa ni kwa Mungu, nikazimia,” asema.

Anasema kwamba ajali hiyo ilikuwa ya saa tano lakini aliamka baada ya muda wa saa tano akiwa katika Hospitali Kuu ya Murang’a akiwa amezingirwa na baadhi ya watu wa familia na marafiki wa bodaboda.

“Nilipofungua macho, nilimwona babangu mzazi amefanya ishara ya msalaba huku marafikiwangu wakishangilia. Wahudumu wa hospitali walikimbia tulipokuwa na wakatuamrisha tunyamaze kwa kuwa tulikuwa tukisumbua wagonjwa wengine,” asema.

Anasema hakuwa akifahamu alikokuwa na kwa nini iwe sherehe akiwa amelalishwa kwa kitanda na ndipo fikira zikamwambia alikuwa akitolewa kafara kwa madhabahu ya kishetani…

“Niliruka kutoka kwa kitanda nikiwa tayari kupambana kufa kupona ili nijinusuru. Lakini waliokuwa hapo wakanishika na kuniweka kwa kitanda… Ndipo wakaanza kuniambia nilihusika katika ajali nikielekea Kabuta… Nikaanza kurejelewa na fahamu… Nikauliza nini kilifanyika,” asema.

Anasema ndipo alifahamishwa kuwa aliponyoka mauti katika ajali hiyo lakini yeye akigonga bampa ya lori na kurushwa juu, Bw Kibata alikumbana na mlango wa kulia wa lori hilo na akaaga dunia papo hapo baada ya kupata majeraha kichwani na kwa kifua.

“Nililia. Nilikumbuka kwamba tulikuwa katika mashindano ya Sh200 pekee. Isipokuwa ni upumbavu huo na tamaa ya pesa, hatungejipata katika ajali hiyo. Niliwaambia wanionyeshe kwenye Bw Kibata alikuwa amelazwa na ndipo waliniteremsha hadi kwa upande wa Mochari na nikamwona rafiki yangu akiwa hoi pumzi ya uhai ikiwa imemtoka,” asema.

Wazazi wa Bw  Kibata ambao ni Bw Simon Karongo na Bi Eunice Njeri walipata habari hizo, waliambia Taifa Leo kwamba walihuzunika si haba.

“Mimi nilikuwa nyumbani nikistarehe tu kwa kivuli wakati simu yangu ililia. Kuipokea, sauti upande mwingine ikaniambia nilikuwa nikihitajika kwa dharura katika hospitali ya Murang’a kwa kuwa kijana wangu alikuwa amehusika katika ajali,” akasema.

Bw Simon Karongo ambaye ni babake marehemu Edwin Kibata. PICHA | MWANGI MUIRURI

Anasema aliamka na hata bila ya kubadilisha nguo alizokuwa nazo za kilimo, alianza mbio, njiani akimpigia mke wake aliyekuwa kwa soko mjini Murang’a na akamuagiza wakutane katika hospitali.

“Kufika, nilimpata mke wangu akiwa katika majonzi makuu na hata bila ya kungojea kufahamishwa yaliyokuwa yamejiri, nikang’amua tu. Nilienda kuutazama mwili na nikafanikisha harakati za kuuhifadhi katika mochari ya Murang’a,” asema.

Kwa upande wake, Bi Njeri alisema kwamba alimpoteza kijana aliyekuwa mchangamfu na mwenye bidii ya mchwa.

Bi Eunice Njeri akiongea na mwandishi wa habari Bw Kahara Kairia kuhusu kifo cha Edwin Kibata ambaye alikuwa kifungua mimba wake. PICHA | MWANGI MUIRURI

“Nitamkosa sana kwa kuwa hata alikuwa ameanza kunifichulia kwamba alikuwa katika harakati za kuoa. Asafiri tu salama lakini nawahimiza wenzake katika sekta ya bodaboda wajifunze na mkasa huu wa mwanangu na wakome maamuzi yasiyokuwa ya busara,” akasema.

Babake Kamau ambaye ni Bw John Gathenge alisema kwamba “hii ni mara ya nne huyu kijana wangu kuhusika katika ajali akiwa katika ubishi tu huo wa nani mwenye mbio kuwaliko waendeshaji wengine”.

“Yuko na sifa ya mbio na nimekuwa nikimkanya. Ana bahati sana kwamba katika ajali hii, alipata tu jeraha kwa kidole cha mkono na pia akakwaruzwa mguun,” akasema Bw Kamau.

Bw John Gathee asimulia mwandishi wa habari Bw Kahara Kairia wa Kayu FM jinsi ambavyo amekuwa akimkanya Erastus Kamau ambaye ni mwanaye dhidi ya kushiriki makimbizano ya pikipiki barabarani. PICHA | MWANGI MUIRURI

Bw Kamau alisema kwamba ajali hiyo imemshtua ajabu na hata anawazia kuokoka na akiri Yesu Kristo kama mwokozi wa maisha yake ndani ya imani ya Kianglikana.

“Nahitaji muda tu wa kuwaza na kuwazua na huenda unipate kanisani nikiwa nimeokoka. Nashukuru Mungu kunijalia uhai wangu katika ajali hiyo na ninaapa mbele yake kwamba sitawahi kubishana barabarani tena kwa mbio za pikipiki,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamuziki Muigai wa Njoroge akana ‘kumdhuru’...

Omtatah akosoa Sheria ya Fedha 2023 akidai imejaa ufisadi

T L