• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 9:50 AM
Taasisi 70 za kozi za kiufundi kupigwa jeki ya Sh8.8 bilioni

Taasisi 70 za kozi za kiufundi kupigwa jeki ya Sh8.8 bilioni

NA TITUS OMINDE

SERIKALI kupitia kwa Idara ya Elimu na Mafunzo ya kiufundi itatoa ufadhili wa kima cha Sh8.8 bilioni kwa taasisi 70 za TVET kote nchini.

Ufadhili huo ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa, upanuzi, na ujenzi wa miundomsingi miongoni mwa matakwa mengine.

Katibu katika idara ya TVET Esther Muoria alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa taasisi zote za umma za TVET zimewekewa vifaa vya kisasa.

Hatua hiyo inapania kukabilia na uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi wa kiufundi katika sekta mbalimbali nchini.

Bi Muoria alisema kuwa taasisi nyingi za TVET zinakabiliwa na uhaba wa vifaa, jambo ambalo linatatiza huduma kutoka kwa wafanyakazi wenye ujuzi wa kiufundi.

Alipokuwa akizungumza katika Chuo cha kiufundi cha Kitaifa cha Eldoret Bi Muoria alikariri kujitolea kwa serikali kuhakikisha taasisi za Tvet zina vifaa na mashine bora za kutoa mafunzo ambayo yanaweza kuandana na viwango vya tasnia husika.

“Serikali imeanzisha mpango kabambe wa kununua vifaa vya kisasa vya mafunzo kwa taasisi 70 za TVET kwa gharama ya Sh8.8 bilioni ili kuongeza watu wenye ujuzi tayari kujiunga na soko la ajira,” alisema Bi Muoria.

Katibu huyo alisema hayo katika taasisi ya kiufundi ya Eldoret National Polytechnic katika Kaunti ya Uasin Gishu ambapo aliongoza kufungwa kwa warsha ya siku tatu ya wasimamizi wa taasisi za kitaifa za mafunzo ya TVET, na wafanyakazi wakuu wa kiufundi na wakuu wa idara lengwa kutoka Rift Valley.

Bi Muoria alitoa changamoto kwa wanafunzi kunufaika na mpango wa serikali wa kuzipa taasisi za TVET mashine na vifaa vya hali ya juu ili kutoa mafunzo ya ustadi wa hali ya juu kukimu matakwa ya walengwa na kubuni ajira katika sekta mbalimbali nchini na katika viwango vya kitaifa.

Wizara hiyo inapania kushirikiana na wadau wote kutafutia wahitimu nafasi za ajira katika ngazi ya kitaifa.

“Serikali iko tayari kuwaunganisha wahitimu waliofaulu kutoka taasisi za TVET na soko la ajira ndani na nje ya nchi na pia kuwasaidia kupata mapato kutokana na ujuzi husika,” aliongeza Bi Muoria.

Anasema TVET huwa na jukumu muhimu katika kuwezesha vijana kupata mafunzo ya kiufundi ambayo yatawasaidia kushiriki katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

  • Tags

You can share this post!

Zuchu aweka ua kulinda ngome ya penzi lake

Ni kufa kupona Harambee Starlets wakishuka dimbani dhidi ya...

T L