• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Tume ya haki yakatazwa kushiriki kesi Shakahola

Tume ya haki yakatazwa kushiriki kesi Shakahola

NA BRIAN OCHARO

MANUSURA wa mauaji ya halaiki ya Shakahola wamepata pigo baada ya mahakama kuzuia Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) kushiriki katika kesi hiyo.

Katika kesi hiyo, serikali imeeleza kuwa walionusurika sasa watachukuliwa kama watuhumiwa na kufunguliwa mashtaka — mara tu uchunguzi kuhusu mfungo mbaya, uliopelekea mamia ya wafuasi wa kanisa la Good News Internal la Paul Mackenzie kuaga dunia, utakapokamilika.

Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Shanzu Joe Omido aliamua kwamba ombi la KNCHR kukubaliwa kushiriki kesi hiyo kama mhusika halikuwa na msingi.

“Nina hakika maombi ya sasa hayafai. Tume haijaeleza namna au aina ya hasara itakayopata iwapo mahakama haitaruhusu maombi yake kushiriki katika kesi hii,” alisema Hakimu Omido.

Tume ilihoji kuwa ombi lake lilinuia kuhakikisha kwamba mara tu itakapojiunga katika kesi hiyo kama mhusika, ushahidi wote unaokusanywa wakati wa upelelezi unawasilishwa mahakamani na kwamba ikiwa ushahidi hautakubaliwa basi hautafanikiwa.

Lakini korti ilisema uwasilishaji huo hauwezi kudumu kwani kesi dhidi ya watu hao bado haijaanza, na kwamba korti haitarajii kupokea ushahidi wowote kutoka kwa wahusika katika kesi hiyo.

KNCHR pia ilihoji kuwa kuendelea kuzuiliwa kwa manusura hao bila kufunguliwa mashtaka rasmi, pamoja na ombi la serikali la kuwaweka kizuizini kwa siku 180 zaidi, ni kinyume cha katiba.

Aidha, Tume ilisema serikali imekuwa na ulegevu katika suala hili na hivyo inataka kushiriki kesi ili kutoa msaada wa kisheria kuhakikisha haki inatendeka haraka.

“Tume imekuwa sehemu ya mkasa wa Shakahola katika viwango tofauti ikiwemo kufuatilia ufukuaji, uchunguzi wa maiti na kushiriki kesi mahakamani. Kwa hivyo hatuwezi kupuuzwa,” KNCHR ilisema kupitia wakili Annemarie Okutoyi.

Bi Okutoyi alihoji kwamba Tume inapaswa kuruhusiwa kushiriki kesi baada ya kushiriki katika michakato mbalimbali kuhusiana na mauaji hayo ya kutatanisha.

Hata Hivyo, upande wa mashtaka ulipinga Tume hiyo kushiriki kesi hiyo ukidai KNCHR haikuwasilisha hoja za kisheria kujumuishwa.

Kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Victor Juma, serikali ilisema Tume haijaeleza athari ambazo zingetokea iwapo itanyimwa fursa ya kushiriki.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma, Jami Yamina, aliteta kuingizwa kwa KNCHR katika kesi hiyo akisema tayari serikali inashugulikia kesi hiyo kisheria.

  • Tags

You can share this post!

Kidosho na shemeji waingia mitini baada ya kunaswa na mzee...

Nilimnasa akigawa asali akadai simtoshelezi

T L