• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Ufisadi: EACC yalaumiwa kumulika magavana na kuipendelea serikali kuu

Ufisadi: EACC yalaumiwa kumulika magavana na kuipendelea serikali kuu

NA CAROLINE WAFULA

MAGAVANA watatu wamehimiza Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuangazia ufisadi katika kiwango cha Serikali ya Kitaifa kwa kutumia ari sawia na inayotumika kulenga serikali za kaunti.

Magavana Jonathan Chelilim Bii (Uasin Gishu), Profesa Anyang Nyongó (Kisumu), na Dkt Wilbur Ottichilo (Vihiga) jana walishutumu Tume hiyo wakisema magavana katika kaunti zote 47 wanahisi kuwa vita dhidi ya ufisadi vinapendelea Serikali ya Kitaifa.

Wakuu wa kaunti walisema haya kufuatia ripoti ya EACC, iliyotaja kaunti zinazoongoza kwa ufisadi huku ikifichua kuwa inachunguza kesi 67 za watu maarufu kuhusu ufisadi na ukiukaji wa sheria za ununuzi katika kaunti za Marsabit, Samburu, Wajir, na Mandera.

Mkurugenzi Mkuu wa EACC Twalib Mbarak aliyewasilisha ripoti hiyo kwa Kamati ya Seneti kuhusu Haki na Masuala ya Sheria mnamo Septemba alisema kesi hizo ni sehemu ya kesi 231 kuhusu ufisadi zilizopokewa na kusajiliwa na Tume.

Wakizungumza Eldoret, magavana Bii, Nyong’o, na Ottichilo, vilevile walikosoa mashirika ya kukusanya maoni huku wakiyashutumu kwa kusawiri, kwa njia isiyo ya haki, kaunti kama zilizo fisadi zaidi, kwa kutumia walichotaja kama mbinu zisizo za kisayansi ambazo hazina ushahidi.

Gavana Bii alisema kumekuwa na dhana kuwa kaunti na magavana ndio wafisadi zaidi huku serikali za kitaifa zikidaiwa kuangaziwa kidogo tu.

Alisema Tume hiyo aghalabu imelaumiwa kwa kuandama kaunti na magavana.

Kulingana na Gavana wa Uasin Gishu, ufisadi mwingi hufanyika katika kiwango cha kitaifa hivyo basi EACC inapaswa kuonekana ikikabiliana na suala hilo kwa kutumia nguvu zizo hizo inazotumia kwa kaunti.

“Mitandao sugu zaidi ya ufisadi ipo kwenye viwango vya kitaifa, inaonekana sisi ni vituo rahisi,” alisema katika Boma Hotel, Eldoret ambapo EACC ilikuwa na kikao na kaunti nne kwenye mpango wa uhamasishaji na mafunzo unaolenga kufafanua kazi yake.

“Tafadhali mnapotuadhibu huku chini, tazameni juu vilevile. Tunataka kukuona kuanzia juu kwa sababu jambo hili limegatuliwa na linaanza katika Serikali Kuu,” alisema.

Gavana wa Siaya James Orengo na manaibu wake walisusia mafunzo hayo yaliyowaleta pamoja wafanyakazi wa kaunti na magavana kutoka kaunti za Siaya, Vihiga na Kisumu.

  • Tags

You can share this post!

Shabiki sugu wa Gor na Arsenal ashinda Sh27 milioni za...

Ushuru wa nyumba ni haramu, mahakama yamwambia Ruto

T L