• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Ugumu wa maisha wasukuma wanafunzi wa vyuo kuishi kama mume na mke

Ugumu wa maisha wasukuma wanafunzi wa vyuo kuishi kama mume na mke

NA RICHARD MAOSI

HALI ngumu ya maisha imeshinikiza wanafunzi wa vyuo vikuu nchini na taasisi za elimu ya juu, kuishi kama mume na mke ili kupunguza gharama.

Wanafunzi wa vyuo vikuu, maarufu kama ‘Comrades’, wamechukua hatua hiyo ili kugawanya matumizi ya pesa, kati ya kiume na wale wa kike.

Wamefunga ndoa za mkataba mfupi, na kuwasukuma mabinti wengi kuanza kupanga uzazi hata kabla ya kufikia umri wa kuolewa.

Upangaji uzazi, ni njia mojawapo kujikinga dhidi ya kushika mimba.

Hii ndiyo hali halisi ambayo utakumbana nayo unapozuru nyumba za kukodisha katika mazingira mkabala na vyuo vikuu vya umma na kibinafsi nchini.

Maeneo yaliyopigwa darubini ni Juja, Ngara, eneo la Njoro Kaunti ya Nakuru na Mti Moja viungani mwa mji wa Eldoret.

Asilimia kubwa ya wanafunzi wanaokaa pamoja, walifichulia Taifa Leo Dijitali kwamba ni njia ya kipekee ambayo huwasaidia kumjua na kumwamini mpenzi.

Wanaungama kuwa huleta tumbojoto pale mpenzi anapokaa mbali na mwenzake.

Alice (sio jina halisi) mwanafunzi wa utabibu katika Chuo kimoja jijini Nairobi, anaishi na mpenzi wake huu ukiwa ni mwezi wa sita.

Anasema anashindwa kutofautisha endapo amejiingiza kwenye mapenzi ya kweli au ni tamaa za kimwili.

“Sioni haja baadhi ya vyuo vikuu kupiga marufuku, wanafunzi wanaume kuzuru mabweni ya mabinti nyakati za usiku,” Alice anasema.

Kulingana naye, njia kama hii haitasaidia lolote kwani wengi wao huwa wamefikisha umri wa miaka 18 na wana njia nyingi za kushinda pamoja hasa wikendi.

“Wanafunzi wanaopangisha vyumba nje ya vyuo huwa na uhuru mkubwa wa kufanya lolote walitakalo, ikizingatiwa kuwa wako mbali na walinzi wa shule au wazazi wao,” mwanafunzi mwingine kwa jina John (si jina lake halisi), anasema.

Awali, Taifa Leo Dijitali iliangazia taarifa ambapo wanafunzi wa vyuo wanajihusisha na ukahaba ili kujiendeleza kimaisha.

Aidha, wameripotiwa kuwaibia wateja walevi katika vilabu mbalimbali nchini.

 

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto ‘kuvamia’ tena ngome ya Raila kusaka umaarufu...

Kibra itakuwa sawa na mtaa wa kifahari wa Karen, Ruto aahidi

T L