• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
UHC: Serikali yaambiwa ikome kuwa kupe kwa kutegemea tu wahisani

UHC: Serikali yaambiwa ikome kuwa kupe kwa kutegemea tu wahisani

NA MARY WANGARI

WADAU wa afya wameonya Kenya na mataifa ya Afrika kwa ujumla dhidi ya kuendelea kutegemea zaidi msaada kutoka kwa wahisani wakisema hali hiyo inahujumu juhudi za kufanikisha Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) kufikia mwaka wa 2030.

Ripoti mpya iliyotolewa kuhusu Hadhi ya Ufadhili katika Huduma ya Afya Nchini inaashiria kuwa kiasi cha fedha zinazowekezwa na serikali kwa sekta ya afya nchini ni cha chini mno huku sehemu kubwa ikitoka kwa wafadhili.

Wakizungumza katika Kongamano la 13 la Mtandao wa Afrika Mashariki kuhusu Afya ya Uzazi (EARHN), wataalam walisema kuwa sekta ya afya haipo miongoni mwa sekta tano kuu zinazotengewa kiasi kikubwa cha pesa na serikali licha ya kutumika pakubwa katika kampeni za kisiasa kushawishi wapigakura.

“Ni sharti tuongeze uwekezaji unaotoka humu nchini kwa sekta ya afya. Hatuwezi kuendelea kutegemea wahisani. Ikiwa ni lazima tuwashirikishe, inafaa kuwa katika ngazi za juu na wala si katika masuala kama vile malipo ya mishahara kwa wahudumu wa afya na shughuli za kila siku katika uendeshaji wa sekta za afya,” alisema Mkurugenzi wa Sera na Tafsiri ya Maarifa katika taasisi ya Maendeleo ya Sera Afrika (AFIDEP), Bi Rose Oronje.

Kulingana na Bi Oronje, Wizara ya Fedha nchini imekuwa ikijishughulisha zaidi na maendeleo na ukuaji wa uchumi huku sekta ya afya ikitelekezwa.

“Wakati umewadia kwa nchi za Afrika kutilia maanani rasilimali zao kustawisha mifumo ya afya. Hutuwezi kukuza uchumi na watu wagonjwa. Tulishuhudia wakati wa janga la Covid-19 kwamba wahisani wengi walirejea makwao na kutelekeza nchi walizokuwa wakisaidia.”

Ripoti hiyo vilevile imehimiza serikali kufanyia mageuzi mfumo wa bima ya afya nchini ambao kwa sasa unawafaidi wanajamii wachache tu huku wengi wao wakiachwa nje.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaashiria kuwa watu wapatao 2 bilioni wanakabiliwa na mzigo mkubwa au kutumbukizwa kwenye ufukara kutokana na Matumizi ya Pesa Mifukoni Mwao (OOP) kugharimia matibabu.

Akizungumza katika kongamano hilo lililoandaliwa jijini Nairobi, Afisa Mkuu wa AFIDEP, Clive Mutunga, alisema kuwa huduma za bima ya afya nchini aghalabu zinatolewa na mashirika ya kibinafsi ambapo ni watu wachache tu walioajiriwa hunufaika huku idadi kubwa inayojumuisha wazee, watu wasio na ajira na maskini wakiwa hawana bima ya afya.

“Ukosefu wa usawa katika huduma ya afya ni changamoto kuu na ni sharti suluhu ipatikane kufanikisha UHC kufikia 2030. Mfumo mwafaka wa afya huwalinda raia kutokana na umaskini ambao huenda ukatokana na kutumia pesa zao nyingi kugharimia matatizo ya afya,” alisema Bw Mutunga.

Kenya ni miongoni mwa mataifa manne ikiwemo Uganda, Burundi na Tanzania yanayoongoza kwa viwango vya OOP.

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi South B PEFA Academy wachagua viongozi...

Mukumu: Machogu aahidi fidia ya Sh400,000 kwa kila familia...

T L