• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2023 12:23 AM
Washirika wa Uhuru, Ruto wamenyana leo

Washirika wa Uhuru, Ruto wamenyana leo

LUCY MKANYIKA na DAVID MUCHUI

RAIS Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto leo Alhamisi wanapima umaarufu wao mashinani vyama vyao vinapomenyana kwenye chaguzi ndogo za udiwani katika kaunti za Taita Taveta na Meru.

Chaguzi hizo zinaandaliwa katika wadi za Mahoo iliyoko Taita Taveta na Kiagu katika Kaunti ya Meru.

Kiti cha Mahoo kiliachwa wazi baada ya kifo cha aliyekuwa diwani Ronald Sagurani, mnamo Agosti.

Kando na UDA, kampeni kali katika kinyang’anyiro hicho zilifanywa na vyama vya Jubilee na Jibebe cha aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo. Chama cha ODM hakikuwa na mgombeaji bali kiliamua kuunga mkono Jubilee.

Mgombeaji atakayepeperusha bendera ya UDA katika uchaguzi huo ni Daniel Kimuyu, huku Jubilee ikimsimamisha Donald Fundi ilhali Bw Samuel Obwoge anawakilisha chama cha Jibebe.

Daniel Kimuyu aonyesha cheti chake baada ya kuidhinishwa na UDA kuwania kiti cha udiwani. PICHA | MAKTABA

Kampeni za Jubilee ziliongozwa na Mbunge wa Taveta, Dkt Naomi Shaban, huku aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo John Mruttu akiongoza kampeni za UDA.

Mbali na wanasiasa wa eneo hilo, kampeni hizo pia zilihusisha viongozi wa vyama hivyo akiwemo mwenyekiti wa Jubilee Nelson Dzuya, mwenzake wa UDA Johnson Muthama na Bw Kabogo.

Marehemu Sagurani alikuwa mwanachama wa Jubilee, lakini alikuwa ameanza kuegemea upande wa UDA.

Wakati wa mazishi yake, Dkt Ruto alizuiwa na polisi kuandaa mkutano wa hadhara ikidaiwa ilikuwa ni kwa juhudi za kuepusha ueneaji wa virusi vya corona.

Nacho kiti cha wadi ya Kiagu kilisalia wazi kufuatia kufariki kwa Eunice Karegi, na kimewavutia wawaniaji 10 wakiwemo Samson Kinyua wa Jubilee na Simon Kiambi wa UDA.

Vyama vya Jubilee na UDA vinatumia uchaguzi huo kupima ushawishi wao katika eneo la Mlima Kenya, ambalo lina ushindani mkubwa uchaguzi wa mwaka 2022 ukikaribia kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura wake.

Waziri wa Kilimo Peter Munya amekuwa akiongoza kampeni za mgombeaji wa Jubilee katika Kiagu huku Seneta Mithika Linturi wa Meru akipigia debe mgombeaji wa UDA.

Bw Munya, ambaye chama chake ni Party of National Unity (PNU), aliamua kuunga mkono Jubilee kwenye uchaguzi huo na amekuwa akisisitiza kuwa eneo la Mlima Kenya sharti liungane chini ya uongozi wa Rais Kenyatta na chama chake.

Kwa upande wake, Bw Linturi akishirikiana na Mbunge wa Imenti ya Kati, Kirima Ngucine wamekuwa wakiendesha kampeni kali katika juhudi za kuhakikisha mgombeaji wa UDA ameshinda leo Alhamisi.

Bw Linturi alisema wana matumaini makubwa ya kunyakua kiti hicho.

Kufikia sasa, UDA imetumia chaguzi ndogo katika maeneo mbalimbali ya nchi kupima umaarufu wake dhidi ya vyama vingine vya kisiasa hasa Jubilee na ODM.

Mwaka 2020 chama hicho kilimpigia debe mgombeaji huru Feisal Bader katika uchaguzi mdogo eneobunge la Msambweni, Kaunti ya Kwale, ambaye alifanikiwa kumshinda Bw Omar Boga wa ODM.

Mwanasiasa huyo alikuwa pia akiungwa mkono na Jubilee.

Katika chaguzi ndogo ambazo ziliandaliwa mwaka huu 2021, UDA ilifanikiwa kujipenyeza hata katika ngome ya Rais Kenyatta ya Kaunti ya Kiambu kwa kushinda viti vya ubunge vya Juja na Kiambaa kwa ushirikiano na vyama vinavyoegemea upande wa Ruto.

Chama hicho pia kilishinda viti vya udiwani vya Rurii katika Kaunti ya Nyandarua, London iliyoko Nakuru na Gaturi katika Kaunti ya Murang’a.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto waligeuka mahasimu wakuu wa kisiasa baada ya uchaguzi wa 2017.

Rais Kenyatta kwa sasa amekuwa akionyesha kumpendelea Kiongozi wa ODM Raila Odinga licha ya kuahidi kumuunga mkono Dkt Ruto wakati wa kampeni 2017.

You can share this post!

Unesco yatambua muziki wa rhumba kama turathi kuu

Wakulima wa Kiambu wahimizwa kupanda miparachichi na...

T L