Viongozi wa upinzani walaani kukamatwa kwa Mwanaharakati Boniface Mwangi
KUKAMATWA kwa mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu, Boniface Mwangi, kumezua hisia kali miongoni mwa viongozi wa upinzani, wanaharakati na mashirika ya kijamii, ambao sasa wanaitaka serikali kumuachilia huru mara moja na kukoma kutumia idara za usalama kuwakandamiza watetezi wa haki.
Mwangi alikamatwa Jumamosi Julai 19, 2025, na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) nyumbani kwake Lukenya, Kaunti ya Machakos, na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Pangani, Nairobi.
Polisi walisema wanamchunguza kwa tuhuma za kupanga na kufadhili ‘ugaidi’ uliotokea katika maandamano ya Juni 25, ambayo yaligeuka kuwa vurugu zilizosababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali.
Kiongozi wa chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, aliungana na viongozi wengine kulaani kukamatwa kwa Mwangi akikutaja kama “kitendo cha kimabavu na kinyume na katiba.”
“Ninalaani vikali kukamatwa kwa mwanaharakati Boniface Mwangi. Hii ni serikali ya mabavu inayoogopa ukweli. Hatutakubaliana nayo kamwe,” alisema Kalonzo, akiongeza kuwa amewaagiza mawakili wa upinzani kuhakikisha Mwangi anapata haki zake za kisheria.
Naye kiongozi wa chama cha people’s Liberation Party, Bi Martha Karua, alisema serikali inatumia nguvu kutisha raia wanaoikosoa.
“Hili ni jaribio la wazi la kunyamazisha sauti huru na kuzua hofu miongoni mwa wanaharakati. Hatutaruhusu kampeni ya vitisho dhidi ya raia wa kawaida,” alisema Karua.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu, Kenya Human Rights Commission (KHRC) na Vocal Africa, yametaja hatua hiyo kama ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
Mkurugenzi wa Vocal Africa, Bw Hussein Khalid, alisema Mwangi alipotea kwa saa kadhaa bila maelezo yoyote kabla ya kuthibitishwa kuwa anazuiliwa Pangani.
“Huku si tu kukamatwa – ni utekaji unaofanywa kwa kivuli cha sheria. Tunaitaka DCI imuachilie huru mara moja na kusitisha mashtaka ya kusingiziwa,” alisema Khalid.
Kwa upande wake, KHRC ilisema kuwa tuhuma za ugaidi dhidi ya Mwangi ni “za kisiasa” na kwamba hatua hiyo inalenga kuzima juhudi za wananchi kudai haki na uwajibikaji.
Wakili Bw Paul Muite, alisema kibali kilichotumiwa na maafisa wa DCI kukamata Mwangi kina kasoro kubwa za kisheria.
“Hakuna jina wala cheo cha jaji kilichotajwa. Ikiwa tunazungumzia haki, basi hata kukamatwa kwake hakukufuata utaratibu wa kisheria,” alisema Muite.
Wanaharakati wengine na wananchi kupitia mitandao ya kijamii wamezindua kampeni ya #FreeBonifaceMwangi wakitaka aachiliwe huru bila masharti, wakisema kuwa serikali imeanza kutumia mbinu za kuwatisha wanaopinga sera zake.
Maandamano ya Juni 25 yaliyoandaliwa na vijana wa kizazi cha Gen Z yaliishia kwa maafa, ambapo watu zaidi ya 50 walifariki, mamia wakajeruhiwa, na wengine kukamatwa.
Kwa sasa, Mwangi anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu, huku mawakili wake wakijitayarisha kupinga uhalali wa kukamatwa kwake na kuwasilisha ombi la dhamana.
Mnamo Jumapili asubuhi Julai 20 2025 DCI ilisema kukamatwa kwa Mwangi kunahusiana na madai ya “kusaidia vitendo vya ugaidi” katika maandamano ya Juni 25, 2025.
Ilisema kuwa vifaa vifuatavyo vilipatikana nyumbani kwake Courage Base, Lukenya, Machakos: Simu mbili za mkononi na tarakilishi na katika ofisi yake Mageuzi Hub, Hurlingham wakapata diski, kompyuta mbili, chapa za kampuni (Brave Media Ltd & Courage Ltd), vitabu vya hundi, kitoa machozi na risasi tupu ya milimita 7.62.
Kukamatwa kwake kulitokea siku moja tu baada ya Mwangi pamoja na mwanaharakati kutoka Uganda, Agather Atuhaire, kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) dhidi ya Uganda, Tanzania na Kenya, wakidai ukiukaji wa haki za binadamu na mateso.