NA SHABAN MAKOKHA
MALI ya thamani isiyojulikana ilichomeka Jumatatu usiku, baada ya moto mkubwa kutokea katika mojawapo ya mabweni katika Shule ya Upili ya Mumias Boys Muslim.
Moto huo, ambao ulianza mwendo wa saa 2.20 usiku, uliwaacha mamia ya wanafunzi bila la kufanya, baada ya kuchoma vitabu, vifaa vya malazi, sare na bidhaa nyinginre za matumizi ya kibinafsi.
Uchuguzi wa mwanzo umebaini kuwa moto huo ulitokana na tatizo la umeme katika shule hiyo.
Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Mumias Magharibi, Bw Stephen Muoni, alisema kuwa juhudi za wanafunzi, walimu, polisi na wakazi kudhibiti moto huo hazikufaulu.
“Kwa bahati nzuri, hakuna yeyote aliyejeruhiwa wakati wa kisa hicho kwani wakati moto ulitokea, wanafunzi walikuwa madarasani kwa masomo yao ya jioni,” akasema Bw Muoni.
Moto huo unatokea siku tatu baada ya bweni jingine kuchomeka katika Shule ya Upili ya Sacred Heart Mukumu Girls.
Mara baada ya moto shuleni Mukumu, kulitokea mkasa sawa na huo shuleni Kisumu Boys.