• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 12:05 PM
Vita vya maneno vyazuka kati ya Kang’ata na kamishna

Vita vya maneno vyazuka kati ya Kang’ata na kamishna

NA MWANGI MUIRURI

VITA vya maneno vimezuka kati ya Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata na Kamishna wa Kaunti hiyo Bw Patrick Mukuria kuhusu utiifu kwa amri ya Naibu Rais Rigathi Gachagua ya kupambana na utukutu wa wamiliki wa baa na walevi katika eneo hilo.

Mnamo Jumanne, Bw Kang’ata alitoa taarifa katika mitandao ya kijamii akijitetea kwamba alikuwa amezindua mpango wa kupunguza baa kutoka 3,000 hadi 1,700.

“Lakini tuliowazima kupata leseni za kuhudumu mwaka wa 2023 walishauriwa wakate rufaa na hadi sasa hatujapata malalamiko yao,” akasema katika ujumbe aliochapisha katika ukurasa wake wa Facebook.

Hata hivyo, ujumbe huo ulikinzana na matamshi yake ya hivi majuzi katika runinga ya Inooro aliposema kwamba “tulionyima leseni waliungana na wakaenda mahakamani na kwa sasa tunangojea uamuzi wa korti”.

Kufikia sasa, baa zote zilizokuwa zikihudumu mwaka wa 2022 zikikadiriwa kuwa 3,700 zinaendelea kuhudumu bila vikwazo na nyingine zikiendelea kufunguliwa katika kila pembe ya kaunti huku watoaji leseni wakiwa ni maafisa wa serikali ya kaunti.

Kilichomkera kamishna Mukuria ni pale Bw Kang’ata alitangaza kuwa maduka ya pombe ya makali almaarufu Wines and Spirits hayajapewa leseni za kuhudumu kwa kuwa ruhusa ya maduka hayo kuwa katika biashara hutoka kwa kamati ya kiusalama ya kaunti na ambayo kamishna ndiye huwa mwenyekiti.

Maduka hayo ya pombe kali yamezidi kuongezeka na licha ya kuwa bidhaa hizo hufaa kuuzwa kwa wateja wa kubeba pombe hiyo, huwa wanauziwa na kunywa papo hapo kama katika baa za kawaida.

Huku akionekana kukerwa na hatua hiyo ya Bw Kang’ata ya kumsukumia lawama, Bw Mukuria alilalama kwamba maduka hayo hupigwa msasa na kupewa leseni na bodi ya kudhibiti biashara za pombe ya kaunti “na hakuna pahala ambapo kamati yangu huhusika katika kutoa idhini”.

Bw Mukuria alisema kwamba serikali ya kaunti ndiyo hutoa mwenyekiti katika vikao vya bodi hiyo na pia huratibu masuala ya utoaji leseni kwa maduka hayo.

“Matamshi hayo ya gavana Kang’ata ni ya kukera sana na yaliyo na nia ya kupotosha,” akasema Bw Mukuria.

  • Tags

You can share this post!

Wizara ya Ardhi haijafanya hamasisho la mfumo wa kidijitali...

Mapenzi jamani! Huyu unayempenda anampenda yule

T L