• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Wabunge waelekezwa kwa rimoti ya Ikulu

Wabunge waelekezwa kwa rimoti ya Ikulu

NA WAANDISHI WETU

MAAMUZI ambayo yamekuwa yakifanywa na Bunge la 13 yanaonekana kumfaa Rais William Ruto, hali inayoashiria kwamba asasi hiyo imetekwa nyara na serikali na wabunge sasa wanaelekezwa kwa rimoti ya Ikulu.

Hatua ya idadi kubwa ya wabunge kuunga mkono Mswada wa Fedha wa 2023 licha ya kupingwa na Wakenya wengi ni ishara kwamba, Bunge limepoteza uhuru wake.

Mahojiano yaliyofanywa na Taifa Leo miongoni mwa wabunge 152 yamebaini kuwa idadi kubwa watapitisha Mswada huo unaopendekeza kuongezwa kwa ushuru wa bidhaa muhimu kama vile mafuta, hivyo kuumiza raia.

Karibu wabunge wote wa Kenya Kwanza waliohojiwa walielezea azma yao ya kuunga mkono mswada huo licha ya kuonywa na raia katika maeneobunge yao kutoupitisha.

Kati ya Wabunge 152 waliohojiwa, 61 walisema wataunga mkono ilhali wengine 42 wakisema kuwa watapinga. Wabunge 49, wengi wao wakiwa waasi waliogura Azimio na kutangaza uaminifu wao kwa Rais Ruto, walieleza kikosi cha Taifa Leo kuwa hawajafanya uamuzi.

Muungano wa Kenya Kwanza una wabunge 179 huku wale wanaoegemea Azimio wakiwa 157.

Wengi wa wabunge 28 wa Jubilee wametangaza uaminifu wao kwa Rais Ruto.

Taifa Leo imebaini kuwa, baadhi ya wabunge wa Kenya Kwanza waliokuwa wameapa kupinga Mswada huo tayari wamebadili nia.

Mbunge wa Kenya Kwanza ambaye ameshikilia kuwa atapiga kura ya ‘La’ dhidi ya Mswada huo ni mwakilishi wa eneobunge la Githunguri Gathoni wa Muchomba.

Mbunge wa Mathira Eric Mumbi ambaye awali alikuwa ametangaza kuupinga, amebadili nia na sasa amejiunga na kundi la wabunge wanaoupigia debe.

Alhamisi, Naibu Rais Rigathi alidai kuwa wabunge wote wa Mlima Kenya wanaunga mkono mswada huo, ‘isipokuwa mmoja’. Bw Rigathi alikuwa akirejelea Bi Muchomba.

“Nitaingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwamba nilikataa Mswada unaolenga kuumiza Wakenya,” akasema Bi Wamuchomba.

Mbunge Maalumu John Mbadi anadai baadhi ya wabunge wameamua kuunga mkono Mswada huo baada ya kutishwa na Rais Ruto.

“Wakenya wasitarajie lolote Bungeni. Wabunge tayari wametishwa na wanaimba sifa za Mswada wa Fedha wa 2023 ambao unaumiza Wakenya kwa ushuru,” akasema Bw Mbadi.

Rais Ruto amemtaka Spika wa Bunge Moses Wetang’ula aagize kura kupigwa kwa wazi ili ‘nione wabunge watakaokataa Mswada huo’.

Mrengo wa Azimio ukiongozwa na Bw Raila Odinga, pia umetaka wabunge kupiga kura kwa njia ya wazi ‘ili tuone wabunge watakaosaliti Wakenya.”

Wabunge wa Jubilee ambao tayari wametangaza kuunga mkono Mswada huo ni Bi Sabina Chege (mbunge Maalumu), Aden Keynan (Eldas) na Stanley Muthama (Lamu Magharibi).

Katika eneo la Nyanza, mbunge wa Ugenya David Ochieng’ wa chama cha Movement for Democracy (MDG) ametangaza kuunga mkono Mswada huo.

Mwakilishi wa Wanawake wa Nairobi Esther Passaris (ODM) ametangaza kuwa ataunga mkono. Benki ya Dunia tayari imeonya kwamba, ushuru uliopendekezwa katika Mswada wa Fedha wa 2023, utasababisha kuongezeka kwa bei ya bidhaa muhimu kama vile vyakula.

Kamati ya Bunge kuhusu Fedha imeonya kuwa, Wakenya watalemewa na gharama ya maisha iwapo Mswada huo utapitishwa. Lakini kinaya ni kwamba, wabunge wanaotoa onyo hilo wanaunga mkono Mswada. Iwapo Mswada huo tata utapitishwa, Bunge litaonekana kutekwa nyara na serikali hivyo kupoteza imani ya Wakenya. Spika wa Bunge Moses Wetang’ula amekuwa akitoa maamuzi yanayodhihirisha kuwa Bunge limepoteza uhuru lililopewa na Katiba.

Kwa mfano, Spika Wetang’ula Alhamisi alilazimika kutupilia mbali maamuzi yaliyofanywa na watangulizi wake ili kuhakikisha kuwa Bi Chege, ambaye sasa ni mwandani wa Rais Ruto, anaendelea kuhudumu kama Kiranja wa Wachache Bungeni.

Wabunge wa Azimio mwezi uliopita waliamua Bi Chege atimuliwe kutoka wadhifa huo. Lakini Bw Wetang’ula alikataa kumtimua akidai amezuiliwa na mahakama ya Kiambu. Uamuzi huo unakinzana na ule uliotolewa na mtangulizi wake Justin Muturi ambaye alishikilia kuwa Mahakama haina mamlaka ya kuzuia shughuli inayoendelea Bungeni.

Bw Muturi alisema kuwa mahakama inaweza tu kuingilia kati baada ya shughuli hiyo kukamilika. Bi Chege, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) Kanini Kega wanaaminika kuungwa mkono na serikali kutwaa chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Bw Wetang’ula mwaka jana alilazimika kusalimu amri ya Ikulu na kutangaza mrengo wa Kenya Kwanza kuwa na idadi kubwa ya wabunge Bungeni. Bw Wetang’ula alisema kuwa wabunge wa Azimio waliotangaza uaminifu wao kwa Rais Ruto walikuwa ndani ya Kenya Kwanza licha ya kuchaguliwa au kuteuliwa na vyama vya Upinzani.

Bw Wetang’ula alipindua uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu aliyekuwa amesema kuwa mrengo wa Azimio ulikuwa na idadi kubwa ya wabunge. Rais Ruto wiki iliyopita, alifichua kuwa, ameagiza kamati za Bunge kufanyia marekebisho sheria zinazohusiana na ushuru.

Agizo hilo limefasiriwa na wadadisi kumaanisha kuwa Bunge limepoteza uhuru wake.Kamati za Bunge pia zimekuwa zikionekana kuandama wandani wa Bw Kenyatta kwa madai ya kuhusika na ufujaji wa fedha za umma wakati wa utawala wa Jubilee. Hatua hiyo imezua maswali ikiwa wanasaidia Kenya Kwanza kulipiza kisasi.

Ripoti za Moses Nyamori, Leonard Onyango, Gitonga Marete, Mwangi Muiruri, Martin Mwaura, George Munene na Alex Njeru

  • Tags

You can share this post!

‘Acheni domo mtupe mbinu mbadala za ukusanyaji ushuru’

Wanakriketi wa Kenya waanza Kombe la Afrika kwa kulima...

T L