• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Waititu amezirai nyumbani, wakili aambia korti katika kesi ya ufisadi

Waititu amezirai nyumbani, wakili aambia korti katika kesi ya ufisadi

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu alikosa kufika kortini baada ya kuzirai nyumbani kwake Jumapili usiku.

Hii ni mara ya pili kesi hii ya ulaji hongo ya Sh588 milioni kuahirishwa. Mwaka jana, alidai anaugua corona kesi ikaahirishwa kwa kipindi kirefu.

Bw Waititu aliyekuwa anatakiwa kufika kortini kuendelea na kesi inayomkabili ya ufisadi wa Sh588 milioni.

Gavana huyo wa zamani wa Kiambu ameshtakiwa pamoja na mkewe Susan Wangari.

Akiwasilisha ujumbe wa kuzirai kwa Bw Waititu, wakili John Swaka alimweleza hakimu mwandamizi Thomas Nzioki kwamba mwanasiasa huyo amelazwa katika hospitali ya Aga Khan.

Akasema Bw Swaka, “Samahani Waititu na mkewe Susan Wangari hawajafika kortini leo. Amelazwa katika hospitali ya Aga Khan baada ya kuanguka na kuzirai katika makazi yake jijini Nairobi.”

Wakili huyo aliiomba mahakama msamaha pamoja na upande wa mashtaka uliokuwa umewasilisha mashahidi.

Mahakama ilielezwa Waititu anaendelea na matibabu.

“Waititu yuko na mkewe Susan hospitali anakoendelea kupokea matibabu baada ya kuzirai Jumapili (Juni 4) usiku,” Bw Nzioki alielezwa.

“Nimefahamishwa leo (Jumatatu) kwamba mteja wangu alianguka na kuzirai nyumbani kwake. Alipelekwa hospitali Aga Khan na mkewe Susan Wangari wanaoshtakiwa pamoja,” alisema Swaka.

Akiomba kesi hiyo iahirishwe , Swaka, alisema atawasilisha stakabadhi kutoka hospitali ya Aga Khan kuthibitisha Waititu amelazwa mle.

Pia alisema ripoti ya hospitali itathibitisha siku atakazokaa mle hospitali.

Hakimu  aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 6 ili Swaka awasilishe ripoti ya hospitali.

“Sijakabidhiwa nakala kutoka hospitali8 ya Aga Khan kuthibitisha mshtakiwa  amelezwa mle.Naamuru kesi hii itajwe kesho (leo Juni 6.Washtakiwa wote wanatakiwa kufika kortini,” aliagiza Nzioki.

Kesi dhidi ya Waititu inahusu ufisadi katika utoaji wa zabuni za kukarambati barabara katika Kaunti ya Kiambu baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Waititu anadaiwa alizipa kampuni alizokuwa na ushawishi mkubwa kandarasi za kukarabati barabara ili apewe kiinua mgongo.

Mtaalamu wa kukagua hati kutoka idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) alikuwa ameingia kizimbani kuanza kutoa ushahidi ujumbe wa kuugua kwa Waititu ulipowasilishwa.

  • Tags

You can share this post!

Gor yarejea kileleni baada ya Tusker kulewa magoli ya Wazito

Mahabusu wakodolea macho njaa serikali ikifilisika

T L