NA RICHARD MUNGUTI
WAKURUGENZI saba wa kampuni ya uwekezaji katika ujenzi wa nyumba, wameshtakiwa kwa kosa la kupora zaidi ya Sh1 bilioni za wananchi.
Hakimu mwandamizi Ben Mark Ekhubi alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki kwamba maafisa wa uchunguzi wa jinai wanaendelea kupokea malalamiko ya waathiriwa zaidi.
“Ijapokuwa walalamishi 21 ndio walioandikisha taarifa kwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), walalamishi zaidi wameendelea kufurika kuandikisha taarifa,” akasema Bi Kariuki.
Bi Kariuki alieleza mahakama washtakiwa watafunguliwa mashtaka zaidi kwa vile kiwango cha pesa zilizotwaliwa ni zaidi ya Sh1 bilioni.
Mahakama ilielezwa mashtaka zaidi yanaendelea kuandaliwa.
Walioshtakiwa ni Keeru Ngugi Mucheru, Amos Macharia Maina, Joan Gathoni, Fredrick Kariuki Makumi, Gedion Charagu Mwangi, Shiphira Wantui Kanyinti, Agatha Wanjugu Mwaniki, kampuni zao za NMK Capital Investment Limited, Abide Worth Auto-rent Company na NMK Estate Developers Limited.
Walikanusha mashtaka dhidi yao na kuachiliwa kwa dhamana.
Wakurugenzi hao wamekabiliwa na mashtaka 21 kwamba kati ya Oktoba 28, 2021 na Julai 16, 2023, jijini Nairobi, wakiwa wakurugenzi wa kampuni ya NMK Capital Investment na NMK Estate Developers Limited, walikula njama ya kuwalaghai wananchi zaidi ya Sh45,558,731.
Keeru Ngugi Mucheru pamoja na kampuni ya Bidsworth Auto-Rent Company walimlaghai Michael Walekwa Sh4 milioni wakidai wataziwekeza na kumlipa faida ya asilimia 15 kila mwezi.
Keeru na kampuni hiyo walikana kupokea pesa hizo kati ya Machi 26 na Mei 5, 2023, jijini Nairobi.
Kesi itatajwa Oktoba 16, 2023.