• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Wanachama wa UDA wanaokaidi Ruto kuadhibiwa

Wanachama wa UDA wanaokaidi Ruto kuadhibiwa

NA JOSEPH OPENDA

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kimetisha kuwachukulia hatua za kinidhamu wanachama watakaopatikana wakipinga msimamo wa serikali.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Cleophas Malala, amesisitiza kuwa UDA imejitolea kwa dhati kumuunga mkono kiongozi wake, Rais William Ruto.

Amewaonya wanachama dhidi ya kupigia debe ajenda zinazokinzana na msimamo wa serikali kuhusu masuala mbalimbali akisema wanachama kama hao wamekosa kuelewa mipango ya serikali na manifesto ya chama hicho walichochaguliwa kwa tikiti yake.

“Kiongozi wetu amekuwa akifanya kazi kwa bidii kutekeleza miradi inayolenga kuokoa taifa hili kutokana na uchumi kuzorota lakini tuna wanachama ambao hawaelewi hivi. Wamekuwa wakipinga hadharani misimamo na miradi ya serikali. Hatutastahimili wanachama wa UDA wanaopinga miradi ya serikali. Kuanzia sasa, tutaanzisha mikakati ya ndani kwa ndani kukabiliana na wanachama kama hao,” alitahadharisha Bw Malala.

Alizungumza haya katika uzinduzi wa afisi za chama hicho jijini Nakuru ambapo alisema UDA imebuni mifumo inayopaswa kutumiwa na wanachama kuwasilisha malalamishi, ikiwemo mkutano wa kundi la bunge.

Alisema hatua ya kuahirisha uchaguzi za mashinani ilinuiwa kutoa nafasi kwa usajili wa wanachama zaidi.

Alifichua kuwa majadiliano yanaendelea kwa vyama tanzu vya Kenya Kwanza kuvunjwa ili kuunda chama kimoja.

“Tunataka kuwa na chama kimoja imara sawa na Chama cha Kikomunisti nchini China. Tunashiriki mazungumzo na vyama tanzu ili kuvishawishi kuvunjiliwa mbali vyama na kujiunga na UDA,” alisema.

Kuhusu ushirikiano na Chama cha Kikomunisti cha China, Bw Malala alisema unalenga kuwezesha mchakato wa haki katika uchaguzi kidijitali na usaidizi katika kubuni afisi za kisasa za makao makuu ya UDA.

“Tayari tumenunua ardhi ya kujenga afisi ya kisasa ambayo vilevile itakuwa na shule ya UDA kuhusu uongozi ili kuwapa mwongozo vijana wachanga watakaorithi kizazi cha sasa cha viongozi,” alisema.

Bw Malala alisisitiza msimamo wa chama hicho wa kupinga kura ya maamuzi iliyopendekezwa na muungano wa Azimio la Umoja, akisema mapendekezo yote yatatekelezwa kupitia Bunge.

Gavana wa Nakuru, Susan Kihika naye aliwataka wanachama wanaopinga miradi ya chama hicho kujiuzulu na kutafuta mamlaka mapya kupitia vyama vingine.

Alikashifu upinzani kwa kujaribu kurejesha nchi katika hali ya uchaguzi kupitia kura ya maamuzi.

“Hatuna muda wala nguvu ya kuruhusu wazo la kura ya maamuzi tunaposhughulika na uchumi wetu. Lakini iwapo itafanyika, msimamo wetu utasalia ulivyokuwa wakati wa Mpango wa Maridhiano (BBI),” alisema Gavana Kihika.

Kenya Kwanza ilipinga kura ya maamuzi iliyopendekezwa katika BBI.

Kiongozi wa Wajumbe wa Chama cha Kikomunisti China, Mao Ding Zhi, alielezea kujitolea kwa chama hicho kufanya kazi na UDA.

  • Tags

You can share this post!

COP28: Wanaharakati wakubaliwa kuandamana kupinga matumizi...

Mashirika yapigania haki ya ‘boychild’ visa vya...

T L