• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Watumiaji TikTok kuanza kuchuma hela na zawadi

Watumiaji TikTok kuanza kuchuma hela na zawadi

NA WINNIE ONYANDO

WANAOTUMIA mtandao wa kijamii wa TikTok kwa minajili ya kuendeleza biashara sasa wataweza kujichumia hela kupitia maudhui yao.

Hii ni kulinagna na Mkurugenzi wa Idara ya Sera ya Umma serikalini TikTok Barani Afrika, Fortune Mgwili-Sibanda.

Akizungumza jijini Nairobi, mkurugenzi huyo alisema jukwaa hilo linalenga kuanzisha mfumo ambapo watumiaji wataweza kupata hela au zawadi mbalimbali kupitia maudhui yao.

“Tumezindua mifumo mbalimbali ambapo mtumiaji anaweza kujichumia hela. Kwa mfano, Tiktok series inawaruhusu watumiaji kudai malipo kutoka kwa wafuasi au watu wanaotazama maudhui yao,” akasema Sibanda.

Hata hivyo, alisema mifumo kama hiyo haijashika kasi nchini Kenya na hata mataifa mengine Afrika.

Hatua hiyo itawezekana tu kupitia mfumo kama vile live gift na TikTok series.

Kwa mfano, unapojirekodi ukipika, basi wafuasi wako wanaweza kukutumia zawadi mbalimbali na baadaye unaweza kubadilisha kuwa fedha.

Haya yanajiri miezi michache tu baada ya Rais William Ruto kuzungumza na Afisa Mkuu Mtendaji wa TikTok, Shou Zi Chew kuhusiana na masuala ya kudhibiti maudhui yanayopeperushwa kwenye mtandao huo wa kijamii.

Kumekuwa na mazungumzo yanayoendelea nchini kuhusu ikiwa mtandao huo upigwe marufuku au la.

Baadhi ya watu wanalalama kuwa mitandao ya kijamii inatumiwa na waliopotoka na ambao huweka video za ngono na wengine kujirekodi wakiwa uchi.

Agosti 15, 2023, Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la kutoa ushauri la Bridget Connect Consultancy, Bob Ndolo katika ombi lake kwa Bunge la Kitaifa, aliwataka wabunge kupiga marufuku utumiaji wa TikTok nchini, akisema mtandao huo unachangia kuenea kwa maudhui ya ngono.

Ombi hilo litazingatiwa na kamati ambayo itatoa uamuzi wake baada ya siku 60 (tangu lilipowasilishwa bungeni).

Hata hivyo, mjadala mkali ulishuhudiwa, baadhi ya wabunge wakisema mtandao huo unatumiwa kama chanzo cha mapato kwa watu wengi, wakiwemo vijana.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Walanguzi wa dawa za kulevya wasukumwa jela kula maharagwe

Kuku wageuka dhahabu Desemba 2023

T L